Jumamosi, 3 Agosti 2019

SERIKALI IMETOA MILIONI 100 KUJENGA BWENI LA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM HALMASHAURI YA MJI GEITA

 Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika halmashauri ya Mji Geita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara mkoani Geita ambapo amesema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalum katika kituo Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.
Ole Nasha amesema serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwajengea fursa na mazingira mazuri ya kusoma watoto wenye mahitaji maalum na ndio maana imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia  pamoja na vitabu ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.

“Kwa miaka mingi jamii nyingi zimekuwa zikiwatenga watoto wenye mahitaji maalim, lakini kwa sasa nashukuru tumeendelea kuwawezesha kupata haki yao ya Elimu kama walivyo watoto wengine na kwamba wanaweza kuwa na changamoto za kimaumbile lakini ubinadamu wao upo palepale” amesema Waziri Ole Nasha.
 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na watoto wenye mahitaji maalum (Hawapo Pichani)  baada ya kukagua ujenzi wa bweni la Kituo cha Watoto wenye mahitaji Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.
Amewataka wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kutokatishwa tamaa na changamoto walizonazo za kimaumbile kwani serikali imewawekea mazingira ya kuwawezesha kufika mbali zaidi katika Elimu na kuwataka kuendelea kutumia fursa hizo za kielimu ili kutengeneza maisha yao ya baadaye.

 
“Wanafunzi, mtu hawezi kujua kipaji chako ni kipi lakini serikali inakupa fursa ya kuonyesha kipaji chako, Mhe Rais ametambua uwezo mkubwa wa watu wenye mahitaji maalum na ndio maana siku hizi tunae Naibu Waziri anayeshughulika na watu wenye mahitaji maalum ambaye naye ana changmoto ya ulemavu,” amesema Naibu Waziri.
 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akicheza na watoto wenye mahitaji maalum katika kituo cha Watoto wenye mahitaji maalum cha shule ya msingi Mbugani, Waziri huyo yupo mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu

Awali Mwlimu Mkuu wa Shule ya msingi Mbugani Edwicka Ndunguru
  amemweleza Naibu Waziri kuwa  kituo hicho kilijengwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata haki ya kielimu katika mazingira wezeshi na kuwapa fursa wengi zaidi wenye mahitaji maalum wanaoishi mbali na shule zinazotoa elimu maalum kupata elimu.

Amesema mafanikio ya kuwepo kwa vituo vya watoto wenye mahitaji maalum mbali na kuwawezesha kupata haki yao ya kielimu, pia imewasaidia kujifunza ujuzi mbalimbali, jamii imetambua nakuthamini umuhimu wa wanafunzi wenye mahitaji maaluma kupata Elimu na wengine kufanikiwa kupata kazi katika maeneo mbalimbali.
 
Sehemu ya bweni lilojengwa na serikali katika Kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita

“Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapomaliza hapa wanakua na ujuzi katika fani za ushonaji, ufumaji na useremala, fani hizi zimewezesha baadhi kuajiriwa katika maeneo mbalimbali na wengine kujiajiri” amesemu mwalimu Ndunguru.

 
Kituo hicho chenye vitengo vinne vyenye jumla ya wanafunzi 143 ambavyo ni vitengo vya ulemavu wa akili, Viziwi, ulemavu wa viungo na ulemavu wa macho, mbali ya kuhudumia wanafunzi hao wenye uwezo wa kufika shuleni lakini pia vinahudumia watoto 38 wenye ulemavu wa kiwango cha juu ambao hawawezi kufika shuleni.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni