Katibu Mkuu ameyasema hayo katika mahafali ya Ishirini
na tano (25) yaliyofanyika katika Chuo hicho kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani
ambapo amewataka ADEM kuendelea kusimamia utekelezaji wa Mtaala kwa
ufanisi, kutoa takwimu sahihi za shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule
inayotekelezeka, kusimamia fedha za elimu bila malipo kwa ufanisi.
Eneo lingine ambalo Katibu Mkuu ametaka litiliwe mkazo
ni pamoja na kudhibiti nidhamu za wanafunzi mara warudipo
katika vituo vyao vya kazi.
Dkt. Akwilapo amesema mafunzo ya uongozi na usimamizi
wa Elimu pamoja na Ukaguzi wa Shule ni muhimu katika kuwapa uwezo walimu na
viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi, ufanisi na kwa kujiamini zaidi
hususani katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Amewataka wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko katika
Uongozi na Utawala Bora pamoja na Uthibiti Ubora wa Shule nchini kwa
kutumia ujuzi, maarifa, stadi na mbinu mpya walizozipata katika mafunzo ikiwa
ni pamoja na maarifa waliyoyapata kuyaeneza kwa walimu ambao
hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.