Alhamisi, 14 Desemba 2017

Rais Magufuli asema Serikali iko tayari kulipa madai halali ya Walimu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali iko tayari kulipa madai  ya walimu ambayo wanaidai serikali endapo madeni hayo yatakuwa yamehakikiwa na kuthibitishwa kuwa ni madai halali.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Chama cha Walimu ambao unafanyika katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma Rais amesema anatambua sana shida za walimu  na kuwa serikali yake iko tayari kupatia ufumbuzi changamoto hizo.

Rais Magufuli amesema mpaka sasa tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 56 kulipa madeni ya walimu na  kuwa kila mwezi  serikali imekuwa ikituma ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 18 mpaka bilioni 23 kwa ajili ya   kuwalipa walimu.

Rais Magufuli amewataka walimu na wanafunzi  kukubali kufanya kazi katika vituo wanavyopangiwa mara wanapohitimu, Pia amesisitizia suala la mwalimu kutokuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa fedha yake yote na hivyo amewataka walimu kuzingatia suala hilo.

Akizungumza kabla ya Kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako amewapongeza walimu kwa umoja na mshikamano ambao wamekuwa wakiuonyesha kupitia chama hicho cha walimu.

Chama hicho cha walimu kupitia Risala yao imeeleza kuwa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya Tano katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya Elimu.

Katika mkutano Rais Magufuli aliwaongoza viongozi wengine kuchangisha  fedha kiasi cha shilingi milioni 60 ambazo zitagawanywa kwa walimu zaidi ya 1000 ambao wanashiriki mkutano huo.





Alhamisi, 7 Desemba 2017

Finland yaahidi kuendelea kusaidia Sekta ya Elimu

Jamhuri ya Watu wa Finland imesema itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya Elimu kwenye eneo la ubunifu ili kuhakikisha vijana wanakuwa wabunifu ili kuweza kujiajiri pindi wanapomaliza masomo.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Jamhuri ya watu wa Finland nchini Tanzania Pekka Hukka wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo jijini Dar es Saalam kuhusiana na namna bora ya utekelezaji wa awamu ya pili ya programme ya ubunifu inayotekelezwa na Tume ya Taifa  ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH).

Waziri Ndalichako amesema atahakikisha Wizara yake inasimamia kwa karibu utekelezaji wa programu hiyo ili kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa.
Waziri Ndalichako amesema Serikali inatambua msaada  ambao umekuwa ukitolewa na Finland katika sekta mbalimbali nchini  ikiwemo sekta ya  Elimu na kuahidi kuwa  fedha zitakazotolewa zitatumika kama zilivyokusudiwa.


Programu hiyo ya miaka mitano  inatarajiwa kuanza 2018 na kukamilika 2022.




Jumanne, 5 Desemba 2017

Chuo cha Ufundi Arusha chatakiwa kukamilisha ukarabati ili kuwezesha vifaa vilivyonunuliwa kutumika.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amekitaka chuo cha Ufundi cha Arusha kukamilisha ukarabati na upanuzi wa karakana  zake ili kuwezesha vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa vianze kutumika.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo mkoani Arusha ili kujionea utendaji kazi, ambapo amesisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano imejielekeza katika kuboresha elimu ya ufundi ili kufikia malengo ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Ole Nasha amesema kutokana na umuhimu huo serikali nimeamua kuwekeza katika uboreshaji wa vyuo vinavyotoa Elimu ya ufundi kwa kununua  vifaa vya kisasa na kukarabati miundombinu ya vyuo hivyo ili viweze kuzalisha raslimali watu watakaowezesha nchi kujenga uchumi wa viwanda.

 Naibu waziri amesema chuo hicho kimepata vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kisasa vilivyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 14 kutoka nchini Australia ikiwa ni  sehemu ya jitihadi zinazofanywa na serikali ya kuboresha namna ya utoaji wa elimu ya Ufundi kwa lengo kusaidia kuzalisha vijana wengi wenye taaluma ya kisasa katika ufundi.

Ole Nasha amevitaka vyuo vyote vya ufundi kutambua kuwa vina jukumu kubwa la kuwatengeneza vijana watakaokuwa na weledi na umahiri katika kuchangamkia fursa za kazi zitakazokuwa zikipatikana katika miradi mikubwa ya maendeleo.


Kwa upande wake  Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt. Erick Mgaya amesema vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa vitawezesha kurahisisha zoezi zima la ujifundishaji na ujifunzaji kutokana na kuongezeka kwa udahili. 



Vijana watakiwa kuwa na hofu ya Mungu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema  Mipango ya Taifa haliwezi kufanikiwa bila kuwa na vijana waadilifu,wachapakazi na wenye hofu ya mungu  hivyo amewataka vijana kuzingatia masomo ili kuweza kufikia malengo yanayikusudiwa Katika Taifa.

Waziri Ndalichako amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ibada maalumu iliyifanyika katika kanisa la City Christian Center lililopo Upanga Jijini Dar es Salaam ambapo amesema ili mtu yeyote afanikiwe katika maisha lazima hofu ya mungu iwepo katika maisha ya kila siku.

Waziri Ndalichako amesema vijana wengi wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kufanya mambo ambayo siyo msingi wa maisha kama vile kujiingiza  kwenye makundi ya utumiaji wa dawa za kulevya, uporaji, unywaji wa pombe vitendo ambavyo havina faida na matokeo yake ni kijana kuangamia.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la City Christian City Dkt. Reinwell Mwenisongole amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali UA awamu ya Tano katika kusimamia Elimu ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili katika vyuo vikuu, kujenga na kuboresha miundombinu ya vyuo vikuu kwa lengo la kusaidia kuongeza wataalamu ili kutimiza azma ya serikali ya kufikia uchumi wa viwanda.

Askofu Mwenisongole amesema kanisa la kanisa la Christian Center lilianzishwa mwaka 1978 kwa lengo la kuwasaidia vijana kuwa na hofu ya mungu.




Jumapili, 3 Desemba 2017

Naibu Waziri Ole Nasha aelekeza kuwekwa vituo vya upimaji katika mipaka yote nchini

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameiagiza Tume ya Nguvu za Atomiki kuhakikisha inaweka vituo vya ukaguzi wa viwango vya mionzi kwa bidhaa zote zinazoingia na kutoka nchini katika mipaka yote kwa lengo la kudhibiti mionzi katika bidhaa hizo. 

Naibu Waziri ametoa rai hiyo jijini Arusha alipotembelea Tume hiyo ili kujionea jinsi inavyofanya kazi, ambapo amesema ni muhimu vituo hivyo kuwekwa katika mipaka  ili  kuhakikisha bidhaa zinazoingia na kutoka nchini zinakuwa na viwango vya mionzi inayokubalika kimataifa.

Naibu Waziri Ole Nasha ameitaka Tume hiyo kutokuishia katika kutekeleza majukumu ya kudhibiti na kuhamasisha matumizi bora ya mionzi bali inapaswa kuanza kuangalia namna bora ya kuhamasisha matumizi chanya ya nyuklia kwa maendeleo ya taifa katika nyanja za Afya,  Kilimo,  maji  na teknolojia.

Naibu Waziri Nasha pia  alitembelea na kukagua  maendeleo ya ujenzi wa maabara ya kisasa kwa ajili ya upimaji wa ubora wa vifaa mbalimbali vya mionzi ikiwemo vifaa tiba vya Tume hiyo, maabara hiyo inajengwa na fedha za serikali kiasi cha shilingi bilioni mbili.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya nguvu za Atomiki Brigadia Jenerali Fulgence Msafiri amesema kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi walio na weledi katika Teknolojia ya nyukulia imefanya Taasisi  hiyo kukosa  watumishi kutokana na kuanzishwa kwa vituo vya kudhibiti uingizwaji wa bidhaa katika mipaka ya Rusumo,  Mtukula,  Kabanga, Kigoma,  Tunduma,  Kasumulu na Daraja la Mkapa. 




Jumamosi, 2 Desemba 2017

Dkt. Semakafu: Simamieni Mfumo wa menejimenti ya viashiria hatarishi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Avemaria Semakafu amewataka wakurugenzi wa Idara,  wakuu wa Vitengo na Taasisi zilizo  chini ya Wizara kuhakikisha wanasimamia  mfumo wa menejimenti ya viashiria hatarishi ili kudhibiti vishiria hatarishi vinavyoweza kukwamisha malengo ya Wizara kufikiwa.

Dkt Semakafu amesema hayo mjini Morogoro wakati wa kufunga mafunzo ya menejimenti ya viashiria hatarishi yaliyoendehswa na Wizara hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo  watumishi wa wizara hiyo wa ili kuwa na  uelewa wa namna ya kutambua vikwazo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu yao.

Naibu Katibu Mkuu Semakafu amesema mafunzo hayo  yataiwezesha Wizara  kuwa na mfumo thabiti wa kushughulikia viashiria hatarishi na hatimae kuwa na daftari linaloainisha viashiria hatarishi pamoja na mikakati ya udhibiti.

Aidha Dkt. Semakafu amewataka Washiriki wote kuhakikisha wanafanyia kazi kikamilifu maudhui yaliyopatikana katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na kuzingatia miongozo ya Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Wizara.

Pia amemtaka mkaguzi mkuu wa ndani Anna Mhere kuhakikisha anaweka vigezo vya uchaguzi wa waratibu wa viashiria hatarishi katika idara na vitengo ili kupata waratibu ambao kweli watakwenda kutekelezamajukumu yao.

Mafunzo ya menejementi ya Viashiria hatarishi yalianza Novemba 27 na kukamilika Desemba 2, 2017  ambayo yalihusisha Wakurugezi wa Idara, Wakuu wa  Vitengo ndani ya Wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, na Wakurugenzi wasaidizi wa Wizara.

Wengine walionufaika na mafunzo hayo ni Wakuu wa Vyuo vya Elimu ya Ualimu, Wathibiti Ubora wa shule  Kanda, Wakaguzi wakuu wa ndani wa Wizara na Taasisi, Wakuu wa Miradi na wajumbe wanne kutoka kila idara na  Vitengo vya Wizara.






Alhamisi, 30 Novemba 2017

Chuo Kikuu Huria chatakiwa kupanua wigo wa udahili.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kassim Majaliwa amekitaka Chuo kikuu Hiria nchini kuhakikisha kinaongeza ubora wa utoaji Elimu na kupanua wigo wa udahili kwa wanafunzi wa chuo hicho.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya 33 ya Chuo hicho ambayo yamefanyikia mkoani Singida na kusisitiza kuwa Umuhimu wa Chuo kikuu huria uko bayana katika kuhakikisha malengo ya serikali ya kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda inafikiwa kupitia wataalamu wanaomaliza chuoni hapo.

Waziri Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya Tano inatambua na inaunga mkono juhudi zinazofanywa na uongozi wa chuo hicho huku wakisisitizwa kuzingatia vigezo, taratibu za utoaji wa Elimu iliyo bora ili wapatikane wataalamu ambao ni bora kwa maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali inatambua mchango wa Chuo hicho katika kipindi cha miaka 25 ambapo kimekuwa kikitoa  Elimu katika masafa ya mbali hali ambayo inahitaji mwanafunzi kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili kifikia malengo.

Kutokana na juhudi hizo Waziri Ndalichako ameahidi Serikali itaendelea Kuimarisha miundombinu ya Tehama ili Elimu hiyo ya masafa iweze kuwafikia watu wengi zaidi.
Waziri Ndalichako amewataka wahitimu kutumia vyema ujuzi na kuhakikisha wanaimarisha utendaji kazi katika serikali na hata Sekta binafsi.

Pia amewataka wahitimu kujenga nadhani pamoja na kuwa na ari katika  uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuwa mabalozi katika Shughuli ambazo watakuwa wanazifanya.