Waziri Ndalichako amesema shule ya sekondari Kigoma ni miongoni
mwa Shule Kongwe na tayari Serikali imekwishatoa fedha za kutosha
ambapo ukarabati wa shule ulitarajiwa kukamilika mapema Mwezi
Septemba, 2017 ili shule zitakapofunguliwa Januari 8,
2018 ukarabati uwe umekamilika na wanafunzi waweze kutumia miundombinu hiyo.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Kigoma kwenye
ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi na ukarabati wa shule mbalimbali
unaotekelezwa na Wizara yake kupitia Programu maalumu ya Lipa kulingana na
matokeo.
Kufuatia kusuasusa kwa ukarabati wa shule hiyo ya sekondari
Kigoma, Mkuu wa mkoa wa kigoma Brigadia Jenerali mstaafu Emmanuel
Magaga ameamuru kukamatwa na kuwekwa ndani kwa meneja wa Wakala wa
majengo wa TBA wa mkoa wa Kigoma Mgala Mashaka ili uchunguzi
ufanyike dhidi yake kutokana na kutuhumiwa kujihusisha na miradi binafsi,
pamoja na kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
Akiwa mkoani Kigoma Waziri Ndalichako pia alikagua vifaa vya
maabara ambavyo tayari vimepokelewa kwenye shule mbalimbali za sekondari.