Jumamosi, 10 Februari 2018

Serikali yaridhishwa na ujenzi wa Maktaba ya kisasa UDSM.


Serikali ya Tanzania imeridhishwa na hatua ya ujenzi wa Maktaba ya kisasa pamoja na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa  kujenga Maktaba ya kisasa katika Chuo kikuu cha Dar es salaam ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 2000 na kihifadhi vitabu 800,000 kwa mara moja

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua hatua za ujenzi unavyoendelea Chuoni hapo jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali ya China inatambua vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Tano hivyo wameahidi kuisaidia Tanzania ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vipaumbele vilivyowekwa ikiwemo  Elimu inatimiza malengo yaliyokusudiwa.

Waziri Ndalichako amesema Maktaba hiyo ya kisasa na kubwa barani Afrika pia inajumuisha jengo la Taasisi ya Confucius ambayo imekuwa ikifundisha lugha na tamaduni za kichina kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam  na watanzania, jengo hilo pia linakumbi za Mubashara, pia vyumba vyenye kompyuta za kisasa zenye programu maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya China hapa nchini Wang Ke amemhakikishia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kuwa nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzani katika maeneo mbali ikiwemo Sekta ya Elimu.

Ujenzi wa Maktaba hiyo unaotarajiwa kukamilika Julai 2018 utagharimu  dola za kimarekani 41,280, 000.




Jumatatu, 5 Februari 2018

Waziri Ndalichako azindua Bodi ya Ushauri ya ADEM na kuitaka Bodi hiyo ifanye kazi kwa weledi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekolojia Profesa Joyce Ndalichako  leo amezindua bodi ya ushauri ya wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) ambapo ameitaka bodi  hiyo iisaidie ADEM kutimiza majukumu yake ipasavyo  kwa upande wa kutoa mafunzo, nidhamu ya utendaji kazi na kusimamia vyema matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo hii leo Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa anategemea kuona matokeo chanya kutoka kwenye bodi hiyo kwa kuwa wote walioteuliwa wamebobea katika masuala mbalimbali yanayohusu Elimu.

Akizungumza mara baada ya maelekezo ya Waziri Mwenyekiti wa bodi hiyo Dk.Naomi Katunzi amemhakikishia Waziri Ndalichako kuwa bodi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia kanuni,  taratibu na miongozo iliyopo.

Dk. Katunzi amesema kuwa wamepokea kwa mikono miwili uteuzi huo na kuwa watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu Kati ya bodi na uongozi wa ADEM.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu  Dk. Joseph Masanja amesema  bodi hiyo  itaishauri  ADEM katika masuala mbalimbali ili kufikia malengo yanayokusudiwa.


Bodi hiyo ambayo imezinduliwa leo itatekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka Mitatu.




Ijumaa, 2 Februari 2018

Katibu Mkuu Mkwilapo asisitiza kuzingatiwa kwa taratibu za manunuzi wakati wote wa ukarabati na ujenzi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk.Leonard Akwilapo amewataka Wakuu wa Vyuo vya Ualimu, Maboharia na Wahasibu wa Wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia taratibu za manunuzi wakati wote wa ukarabati na ujenzi wa Miundombinu ya vyuo  8 vya Ualimu unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. 

Dk.Akwilapo amesema hayo leo mkoani Dodoma wakati wa semina Elekezi kwa watendaji hao juu ya namna bora ya kutumia Force Akaunti wakati wa ujenzi kwa kutumia wataalamu na vifaa vyake au kwa  kukodi na kutumia mafundi wengine.

Dk. Akwilapo amewasisitiza wakuu hao wa vyuo vya Ualimu kuhakikisha wanatunza vyema kumbukumbu za matumizi ya fedha, ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ambazo zitasimamia manunuzi, upokeaji wa vifaa na matumizi bora ya vifaa hivyo.

Awamu hii ya pili inahusisha Chuo cha Ualimu Patandi, Tarime, Nachingwea, Murutunguru, Mangaka, Tandala, Ilonga na Kinampanda ambapo tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa kulingana na Matokeo imeshatuma fedha za awali   kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa ajili kazi hiyo.


Awamu ya kwanza ya ukarabati ilihusisha  Vyuo vya Ualimu 10 ambavyo ni  chuo cha Butimba, Mpwapwa, kleruu, Songea, Kasulu, Tukuyu, Korogwe, Marangu, Morogoro na  Chuo cha Tabora ambapo Wizara ilitumia shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo hivyo.






Jumamosi, 27 Januari 2018

waziri Ndalichako asisitiza michango ya hiari haijakatazwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali haijakataza uchangiaji wa hiari na kuwa kilichokatazwa ni michango ya lazima ambayo imekuwa kero kwa wazazi kwani imekuwa kama kiingilio, ambapo mtoto haruhusiwi kuingia shuleni kabla mzazi hajalipa michango hiyo.

Waziri Ndalichako amesema Serikali haizuii wananchi kwa hiari yao wenyewe kuchangia Maendeleo ya Elimu ya watoto wao iwapo michango itakusanywa kwa utaratibu uliowekwa na kuratibiwa na mmoja wa wazazi na siyo mkuu wa shule.

Waziri Ndalichako ametoa kaui hiyo mjini Makambako mkoani Njombe wakati akishiriki uzinduzi wa kampeni ya upimaji wa kansa ya matiti na mlango wa kizazi, kifua kikuu na magonjwa mengine yasiyoambukiza kampeni ambayo iliratibiwa na mkoa huo wa Njombe.

Akikagua ujenzi wa mabweni unaoendelea katika shule ya sekondari Sovi iliyopo mkoani Njombe Waziri Ndalichako amekiri kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mabweni hayo ambapo aliwasifu wananchi kwa kazi nzuri inayofanywa na viongozi wao wa mkoa.

Waziri Ndalichako amewataka wananchi kuendelea na moyo wa kuchangia Ujenzi huo na kamwe wasikatishwe tamaa na uvumi uliopo kuwa hawaruhusiwi kuchangia maendeleo yao ya Elimu ya watoto wao.

Akiwa Wilayani Makete Waziri Ndalichako aliamrisha kusimamishwa Ujenzi wa chuo cha ufundi stadi VETA kwa kuwa gharama zilizotajwa zipo juu sana na hazina uhalisia, ambapo amemuagiza Meneja wa VETA wa kanda kwa kushirikiana na mhandisi wa Halmashauri asimamie ili gharama hizo ziangaliwe upya.

Waziri Ndalichako alisikitishwa kuona ujenzi haujaanza mpaka sasa japo kuwa mkataba wa kazi hiyo ulisainiwa Agosti, 2017 na kazi ya Ujenzi kukabidhiwa kwa Mkandarasi ambaye ni Wakala Wa Majengo - TBA Oktoba 2017.

Pia Waziri Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonrd Akwilapo kutuma Mkaguzi ili afuatile matumizi ya fedha ya mradi huo.





Ijumaa, 26 Januari 2018

Profesa Mdoe: Stadi za Kazi zinachangia Maendeleo ya Viwanda

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa James Mdoe amesema Taifa letu haliwezi kufikia malengo ya kuwa nchi ya Kipato cha Kati hadi itakapoweza kuwezesha watu kuwa na stadi za kazi ili waweze kuchangia maendeleo ya viwanda na uchumi kwa ujumla.

Prof. Mdoe amesema hayo wakati akifungua mafunzo  ya siku mbili yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kuhusu Uandishi wa Miradi ya Kuendeleza Stadi za Kazi, kwa waajiri na vyuo vya mafunzo kuanzia ngazi ya ufundi stadi hadi vyuo vikuu chini ya mradi wa kukiza stadi hizo (ESPJ).

Profesa Mdoe amewaambia Washiriki hao kuwa lengo la kuwepo Mradi wa ESPJ ni kufanya maboresho katika mifumo ya uboreshaji wa mafunzo ya stadi za kazi (Strengthening the institutional capacity of the skills development system) na kuongeza idadi na ubora wa wahitimu wa mafunzo ya stadi hizo kulingana na mahitaji ya soko la ajira katika sekta zenya kukua kwa haraka.

Prodesa Mdoe amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Sekta Binafsi ili kuviwezesha vyuo kuanzisha au kuboresha programu za mafunzo zinazoendana na mahitaji ya sekta binafsi.

Kwa upande wake mratibu wa Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (ESPJ) Dk. Jonathan Mbwambo, alisisitiza kuwa tofauti na utaratibu wa kuomba na kupangiwa fedha kwa ajili ya mafunzo, mfumo  huu unawataka watoa mafunzo kuandika miradi ya kuendeleza stadi za kazi na kuziwasilisha serikalini ili kuchambuliwa na miradi itakayoshinda kupatiwa fedha.


Mafunzo hayo ya Siku mbili yalijumuisha washiriki 67 na yaliyoratibiwa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Benki kuu ya dunia.




Jumatatu, 22 Januari 2018

Wizara ya Elimu yatoa msimamo kuhusu Shule kufukuza Wanafunzi kwa kutofikia wastani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa wamiliki wa shule binafsi za sekondari ambapo kwa pamoja  wamejadili utekelezaji Wa waraka Namba. 7 unaokataza wanafunzi kufukuzwa shule kwa sababu ya kutofikisha wastani wa ufaulu uliowekwa na shule.

 Waziri Ndalichako ameeleza ameeleza kuwa chimbuko la waraka huo ni baadhi ya shule kufukuza idadi kubwa ya wanafunzi wakiwa Mwaka wa mwisho wa masomo yao kwa kigezo cha kutotimiza wastani unaotakiwa kitendo ambacho amekielezea kuwa kuwa ni cha kibaguzi na ki-unyanyasaji. 

" Mfano  shule ya sekondari Pandahil ambayo imefukuza watoto 148, shule ya sekondari star high imefukuza wanafunzi 49 hizo ni baadhi tu, Aidha, ameeleza kuwa   Wakati Bunge na Serikali ikisikitika pale Wasichana wanapopata uja uzito na kuacha shule, Waja sekondari na Musindi sekondari zimefukuza wanafunzi wa kike 15 kila moja kwa kigezo cha ufaulu mdogo.

Waziri huyo amesisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa waraka huo na amewataka Viongozi hao kuweka utaratibu mzuri kwa wanafunzi walio na uwezo mdogo badala ya utaratibu uliopo sasa wa kuwafukuza shule na hivyo kuwaacha wakiwa hawana pa kwenda.

Kwa upande wao viongozi wa wamiliki wa shule wameeleza kuwa utekelezaji wa waraka huo utasababisha kushukuka kwa Ubora Wa ufaulu katika shule zinazomilikiwa na watu binafsi.


Kikao hicho pia kilihudhuriwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo kikao ambacho kimefanyika jijini Dar es salaam.



Jumamosi, 20 Januari 2018

TBA yapewa wiki moja kuanza ujenzi kampasi ya Mloganzila

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameipa wiki moja  Wakala wa Majengo nchin- TBA- Kuhakikisha ujenzi wa majengo mbalimbali  unaanza mara moja ikiwa ni pamoja na kuongeza mafundi pamoja na kupeleka vifaa vya ujenzi katika Mradi wa  Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.

Prof.  Ndalichako ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa, hosteli, ofisi na bwalo la Chakula katika Chuo Kikuu hicho kilichopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambapo amesema hajaridhishwa na kasi ujenzi huo.

Waziri Ndalichako amesema Wizara tayari ilishaipatia TBA kiasi cha shilingi bilioni 3.9 kama malipo ya awali lakini mpaka sasa hakuna jengo lolote ambalo limeshaanza kujengwa na wala hakuna vifaa vya ujenzi katika eneo hilo zaidi ya kuchimbwa misingi tu.

Waziri Ndalichako amesema hatavumilia kuona udahili wa  wanafunzi wa fani za Afya unachelewa katika kampasi hiyo kwa kuwa  lengo la serikali ni kuongeza idadi ya wanafunzi wa fani hizo nchini.


Naye Kaimu Meneja wa Mkoa kutoka TBA Manase Kalage amemwakikisha Waziri kuwa maagizo aliyoyatoa watayatekeleza ikiwa ni pamoja na kukamilisha mradi huo kwa wakati.