Serikali ya
Tanzania imeridhishwa na hatua ya ujenzi wa Maktaba ya kisasa pamoja na
kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kujenga Maktaba ya
kisasa katika Chuo kikuu cha Dar es salaam ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua
wanafunzi zaidi ya 2000 na kihifadhi vitabu 800,000 kwa mara moja
Akizungumza mara
baada ya kutembelea na kukagua hatua za ujenzi unavyoendelea Chuoni hapo jijini
Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
amesema Serikali ya China inatambua vipaumbele vya Serikali ya awamu ya Tano
hivyo wameahidi kuisaidia Tanzania ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vipaumbele
vilivyowekwa ikiwemo Elimu inatimiza malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Ndalichako
amesema Maktaba hiyo ya kisasa na kubwa barani Afrika pia inajumuisha jengo la
Taasisi ya Confucius ambayo imekuwa ikifundisha lugha na tamaduni za kichina kwa
wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam na watanzania, jengo hilo pia
linakumbi za Mubashara, pia vyumba vyenye kompyuta za kisasa zenye programu
maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake
Balozi wa Jamhuri ya China hapa nchini Wang Ke amemhakikishia Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kuwa nchi yake itaendelea
kuisaidia Tanzani katika maeneo mbali ikiwemo Sekta ya Elimu.
Ujenzi wa Maktaba hiyo unaotarajiwa kukamilika Julai 2018
utagharimu dola za kimarekani 41,280, 000.