Jumatatu, 26 Februari 2018

China na Korea kuisaidia Tanzania katika Sekta ya Afya na Elimu.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichoko ameishukuru Serikali ya Watu wa China kwa kukubali ombi  lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli la kufadhili  wataalam wa sekta ya Afya.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo hii leo alipotembelewa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke aliyefika katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo kuhusu utaratibu wa kupata wanafunzi watakaofaidika na ufadhili huo.

Balozi Wang Ke amesema baada ya Rais wa China kupata maombi hayo ametoa ufadhili wa Serikali yake kwa wanafunzi 20 wa Kitanzania watakaopata ufadhili wa masomo katika Sekta ya Afya kutoka Serikali ya China kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019 katika ngazi za Uzamili na Uzamivu.

Aidha, Balozi Wang Ke amesema mbali na ufadhili huo pia Serikali ya China itaendesha Mpango wa Mafunzo kwa wataalamu wengine 20 mpaka 30 wa Sekta ya Afya kwa muda wa mwezi mmoja nchini China, hivyo amemuomba Waziri  wa Elimu kusaidia katika kuratibu upatikanaji wa Wanafunzi na aina ya mafunzo ambayo yatasaidia katika kutatua changamoto katika Sekta ya Afya.

Katika hatua nyingine Waziri  Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea Song Geum – Young  kwa lengo la kujadili ujio wa wabunge kutoka Bunge la Korea kwa ajili ya kutoa msaada katika Hospitali ya Tiba na Taaluma ya Mlongazila.

Waziri Ndalichako amemwambia balozi huyo kuwa Serikali bado inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga mbiundombinu ya kuwezesha wanafunzi na wauguzi kuishi karibu na hospitali ya Taalum na Tiba ya Mlongazila. 

Waziri amesema kwa sasa serikali ipo katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya Miundombinu itakayowezesha wanafunzi wapatao 1500 kuishi karibu na hospitali hiyo. 

Waziri Ndalichako amesema Hospitali hiyo imejengwa kwa lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi mpaka kufikia wanafunzi zaidi ya 10,000 hivyo bado Miundombinu itakayowezesha kuchukua idadi hiyo ya wanafunzi pamoja na watumishi wa hospitali hiyo inahitajika.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Korea amesema serikali yake bado itaendelea kusaidia katika uendeshaji wa hospitali hiyo pamoja na miradi mingine katika Sekta ya Elimu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Korea  Song Geum – Young ofisini kwake ambapo kwa pamoja walijadiliana namna bora ya kuisaidia uboreshaji wa Miundombinu ya Hospitali ya Tiba na Taaluma ya Mloganzila.




 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako akizungumza na Balozi wa China Wang Ke kuhusu ufadhili wa masomo katika Sekta ya Afya kutoka Serikali ya China kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019 katika ngazi za Uzamili na Uzamivu. 






Alhamisi, 22 Februari 2018

Waziri wa Elimu ashiriki kuaga mwili wa Akwilina Akwiline.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako leo ameongoza Wananchi mbalimbali kuaga mwili wa aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT) marehemu Akwilina Akwiline jijini Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa kumuaga Marehemu Akwilina Waziri Ndalichako amesema msiba huo umemgusa kila Mtanzania kwa kuwa Marehemu amekutwa na umauti akiwa anatekeleza majukumu yake ya kielimu.

Aidha, Waziri Ndalichako amezitaka Mamlaka zinazohusika kuharakisha kufanya uchungizi ili wale wote watakaobainika kuhusuika na tukio hilo waweze kuchukuliwa hatua  kwa mujibu wa  sheria za nchi.

Viongozi wengine walioshiriki kuaga mwili wa Mwanafunzi huyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad  Yussuf Massauni, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Atashasta Nditiye , Kamanda wa kanda Maalumu ya Dar e salaam Lazaro Mambosasa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo.

Mwili wa Akwilina Akwiline tayari umesafairishwa kuelekea mkoani Kilimanjaro na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho mkoani humo.





Jumanne, 20 Februari 2018

Waziri Prof. Ndalichako aziagiza Taasisi za Elimu kufuata Taratibu, Kanuni na Sheria za nchi


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi zinazotoa Elimu ya Juu hapa nchini kufuata taratibu, Sheria na kanuni za nchi katika kuendesha Taasisi hizo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo hii leo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza katika Chuo Kikuu cha Kampla kilichopo Gongo la Mboto  ambapo amebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya watumishi ambao hawana vibali vya Makazi  na Ajira.
Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kumekuwa na udanganyifu wa taarifa za kiutumishi ambapo watu walioajiriwa kama madereva na wahudumu wamekuwa wakiingizwa katika orodha ya watumishi  ambao ni Walimu huku wakijua watumishi hao hawana sifa za kuwa Walimu.

Waziri Ndalichako amesema baadhi ya walimu katika chuo hicho kutoka nje ya nchi wanakuja kama wanafunzi lakini wakifika Chuoni hapo wanahalalishwa na kuwa walimu ambao wanafundisha wanachuo bila kuwa sifa stahiki.

Profesa Ndalichako pia amekitaka chuo hicho kuhakikisha kinafuatilia kwa karibu nidhamu ya wanafunzi wanaosoma Chuo hapo kwa kuhakikisha wanazingatia na kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi.

“Nidhamu ni jambo la msingi sana, sasa hakikisheni wanafunzi wanaomaliza katika chuo hiki wanakuwa na nidhamu ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni na taratibu za ndani  na nje ya nchi na siyo vinginevyo, maana kuna baadhi ya wanafunzi ambao nyaraka zinaonyesha wamemaliza kwenye Chuo hiki na wako nje ya nchi lakini hawana maadili, liangalieni hili kwa umakini,”alisema Profesa Ndalichako.

Kwa upande wake  Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dk. Anna Makakala  amezitaka Taasisi zote za Elimu nchini kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwa ofisi hiyo ili kuepuka kukiuka taratibu na miongozo iliyowekwa na nchi.




Jumatatu, 19 Februari 2018

TAARIFA KWA UMMA



TAARIFA KWA UMMA
Nimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa ya kifo cha Akwilina  Bafhata Akwiline aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Usafirishaji (NIT).
Kifo hicho kimetokea wakati askari wakiwa wanadhibiti maandamano yaliyokuwa yakifanyika tarehe 16/02/2018 kwenye eneo la Mkwajuni Wilaya ya kinondoni, jijijini Dar es salaam.

Napenda kutumia fursa hii kutoa pole sana kwa Familia ya Ndugu,  jamaa na marafiki wote wa Akwilini.  Pia napenda kutoa pole kwa Uongozi na Jumuia ya Chuo cha Usafirishaji, wanafunzi wote nchini na wananchi wote kwa ujumla.

Ndugu Akwilini ni binti aliyekuwa anatambua na kuthamini umuhimu wa Elimu, na alijitoa kuhakikisha kuwa anasoma kwa bidii kwa manufaa yake binafsi, familia yake na kwa manufaa mapana ya taifa taifa.  Kifo chake kimetokea wakati akiwa kwenye kutekeleza wajibu wake kama mwanafunzi wa kupeleka barua mahali alipokuwa anatarajia kufanya mazoezi kwa vitendo yatakayoanza tarehe 27/02/2018. Kifo hicho cha kusikitisha kimezima ndoto yake Serikali ikekipokea kwa masikitiko makubwa sana. 

Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Joseph Pombe Magufuli amesikitishwa  na kuhuzunishwa sana na kifo cha mwanafunzi Akwilini na anaungana na familia, ndugu jamaa na watanzania wote kuwapa pole za dhati kutokana na msiba huo. 
Serikali inatumia fedha nyingi kuwasomesha wanafunzi kuanzia Elimu msingi, sekondari na hutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kwa sababu tunatambua mchango wa Elimu katika maendeleo ya nchi yetu. Marehemu Akwilini alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. 

Mimi  Waziri mwenye dhamana ya  sekta ya Elimu nimesikitika sana kuona binti huyo amepoteza maisha yake akiwa katika kutekeleza shughuli za kielimu.

Wizara yangu itagharamia shughuli zote za mazishi ya Marehemu Akwilina hadi hapo atakapopumzishwa katika makao yake ya milele. 
Namuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo kusimamia shughuli zote za msiba huo hadi  Akwilina atakapozikwa katika nyumba yake ya milele. 

Nitumie fursa hii kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwafikisha mara moja wahusika waliosababisha kutokea kwa tukio hilo kwenye vyombo vya sheria ili  wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Nawasihi sana watanzania wenzangu tujiepushe kukiuka tarataibu na miongozo inayokuwa inatolewa ikiwemo  maandamano na vitendo vyote ambavyo vinaweza kusababisha maafa kwa watu wasio na hatia.

Mungu aiweke roho ya Marehemu Akwilini mahala pema peponi Ameni

Imetolewa na:

Prof Joyce Lazaro Ndalichako
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia.
18 / 02/2018


Katibu MKuu Akwilapo: awataka watumishi wa wizara yake kufanya kazi lea bidii na weledi


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii na  kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Dk. Akwilapo ameyasema hayo wakati wa kikao cha kwanza cha watumishi wa wizara hiyo kilichofanyika mkoani Dodoma tangu serikali itangaze rasmi kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani humo.

Dk. Akwilapo amesema utii, ushirikiano,bidii na upendo mahali pa kazi miongoni mwa watumishi ndiyo silaha pekee ya kufikia malengo ambayo Wizara imejiwekea katika kuinua Sekta ya Elimu hapa nchini.

"Nipende kuwapongeza watumishi wote kwa kushiriki majukumu mbalimbali ya Wizara ikiwemo kuisimamia vyema miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara, nawasihi sana tuusifanye kazi kwa kujitenga, ushirikiano miongoni mwetu ni jambo la msingi sana na tukiwa na Umoja basi mafanikio lazima yatapatika katika Sekta hii ya Elimu,"alisema Dk.Akwilapo.

Pia Katibu Mkuu Dk.Akwilapo amewataka watumishi kuwa na matumizi sahihi ya Teknolojia,kujibu barua mbalimbali kwa wakati pamoja na kushughulikia faili zinazofika kwenye ofisi zao ndani siku mbili  na siyo kuziacha zikae muda mrefu.


Kupitia kikao hicho watumishi pia walipata fursa ya kuwaaga viongozi ambao walitumikia Wizara hiyo ambao hivi sasa wamehamiahiwa Wizara nyingine na kuwakaribisha viongozi wapya ambao wamehamia kwenye Wizara hiyo.

Viongozi waliokaribishwa ni pamoja na Naibu Waziri William Ole  Nasha na Naibu Katibu Mkuu Profesa  James Mdoe na walioagwa ni Naibu Waziri Mhandisi Stella Manyanya na Profesa Saimon Msanjila ambaye hivi sasa ni Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Madini.





Alhamisi, 15 Februari 2018

TBA yatakiwa kulipa madeni ya wananchi katika ujenzi shule ya wavulana Ihungo


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka wakala wa majengo nchini TBA kulipa madeni wanayodaiwa na Wananchi mbalimbali kufuatia ujenzi unaoendelea wa Shule ya Sekondari wavulana Ihungo iliyopo Wilayani bukoba mkoani kagera.

Waziri Ndalichako amesema kuwa tayari wizara imekwisha ilipa TBA  zaidi ya bilioni Tisa na garama ya ujenzi kwa mradi wote ni shilingi  bilioni 10 nukta 48.

" Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni,  nipende kuwapongeza Wakala wa Majengo TBA kwa kazi nzuri ambayo wameifanya.

"Lakini nasikikitika sana kupokea malalamiko kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa inayoeleza kuwa bado kuna Wananchi wanaidai TBA kutokana na kutoa vifaa mbalimbali vya ujenzi kama vile mbao, matofali, na vibarua ambao wameshiriki katika ujenzi huo wa shule ya wavulana Ihungo na kuwa mpaka sasa hawajalipwa, hii haipendezi ni vyema TBA kuhakikisha inalipa madeni hayo,"alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako amesema haoni sababu kwa nini wananchi hawajalipwa wakati tayari Serikali imekwisha ilipa TBA, ni vyema wakalipwa ili kusaidia kuepusha migogiro isiyo ya lazima baina ya Serikali na wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa TBA mkoa wa  Kagera Salum Chanzi amekiri kuwepo kwa sababu mbalimbali zilipelekea mradi kutokamilika kwa wakati na hivyo kuomba wapewe muda zaidi mpaka mwezi machi mwaka huu ili waweze kukamilisha.

"Mheshimiwa Waziri mradi huu haijakamilika kwa wakati uliokuwa umepangwa kutokana na changamoto ya kuagiza vifaa kutoka nje ya mji wa bukoba, na hii inatokana na bei wakati mwingine kuwa kubwa hapa bukoka  lakini nje ya hapa tunavipata kwa bro nafuu," alisema Chanzi.

Chanzi amemhakikishia Waziri Ndalichako kuwa tayari madeni yote wanayodaiwa na wananchi katika ujenzi huo wa Ihungo Sekondari yamewasilishwa kwenye Taasisi yake yanafanyiwa kazi na wahusika wote  watalipwa.