Jumanne, 17 Aprili 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz



Chuo cha Masomo ya  Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA.           




Tarehe: 17 Aprili, 2018
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU UFANISI KATIKA USIMAMIZI WA UREJESHAJI WA MIKOPO NA UKUSANYAJI WA MADENI NA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

A.    UTANGULIZI
Ndugu Waandishi wa Habari, napenda kutumia nafasi hii kuishukuru kwa dhati Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kufanya ukaguzi huu ambao umeainisha mafanikio na changamoto mbalimbali zilizopo katika Usimamizi na urejeshwaji wa Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Pia namshukuru CAG kwa kuibua changamoto ya kuchelewa kwa mradi wa ujenzi katika Chuo cha Ualimu Ndala pamoja na ushauri wake na mapendekezo kwa ujumla aliyoyatoa yenye lengo la kuhakikisha ufanisi katika usimamizi na matumizi ya fedha za umma kwa Wizara na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yangu, unaimarika.

Jumatatu, 16 Aprili 2018

SERIKALI YAAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO KWA WANAFUNZI WENYE UZIWI


Waziri wa Elimu, Sayasni na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amekihakikishia Chama cha walimu Viziwi kuwa Serikali iko tayari kusikiliza na kujua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye uziwi ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa.

Waziri Ndalichako amesema hayo leo mkoani Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na walimu wenye Uziwi ambapo amewaeleza kuwa hajafurahishwa na matokeo ya kidato cha Nne ya shule ya Sekondari Njombe na kubainisha kuwa ni vyema changamoto zikaainishwa ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  akisalimiana na Mkurugenzi wa Chama cha Walimu wenye uziwi Tanzania Karim Bakari.

Kwa upande wake mratibu wa chama hicho cha Walimu Viziwi Francis Mbisso ameiomba Serikali kutoa semina kwa walimu wanaofundisha wanafunzi Viziwi ili  walimu waweze kuelewa saikolojia ya wanafunzi pale wanapowafundisha, lakini pia kuwe  na wigo mpana  wa mafunzo ya ufundi kwa wanafunzi hao  badala ya kuwalazimisha kusoma masomo ya darasani.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akutana na kufanya mazungumzo na Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania. Mazungumzo hayo yanalenga kutataua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye uziwi.

Mbisso ameshauri kuwepo kwa mtaala wa lugha ya alama pekee utakaowasiadi wanafunzi wenye uziwi kuelewa kwa uarahisi masomo yao wanapokuwa darasani ikiwa ni pamoja na kuongeza muda ya kipindi darasani ukilinganisha na muda wanaotumia wanafunzi wa kawaida.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akisalimiana na Mwalimu Theresia Nkwera mwenye uziwi, ambaye alishiriki majadiliano ya pamoja yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye uziwi.

Jumatatu, 9 Aprili 2018

UJENZI CHUO CHA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI CHA MKOA WA KAGERA KUANZA OKTOBA 2018


Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodutus Kinawiro amesema tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa Miundombinu muhimu ya barabara na umeme katika Kijiji cha Burugo ambapo Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi cha Mkoa wa Kagera kinatarajiwa kujengwa.

Kinawiro amesema hivi sasa Mkoa upo katika kukamilisha miundombinu ya maji  na kuwa tayari suala hilo limewekwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.
Mwakilishi wa Kampuni ya ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) Yang Tao akiwapitisha Watendaji wa Mkoa wa Kagera katika Michoro ambayo wameiandaa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera.


Kukamilika kwa Miundombinu hiyo kunatoa fursa ya kuanza kwa ujenzi wa chuo hicho ambapo Ujumbe wa timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) inayotarajiwa kusimamia ujenzi wa Chuo hicho umetembelea eneo hilo ambapo umekiri kuridhishwa na hatua hizo ambazo serikali imezitekeleza.


Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa Kampuni hiyo Fang Kefeng amesema uwepo wa barabara, umeme na maji katika eneo la mradi utawawezesha kutekeleza ujenzi bila kikwazo  na kuwa tayari wameandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho na kwamba mradi utaanza mara baada Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuridhia michoro iliyoandaliwa kwa ajili ya Chuo hicho. 
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Mhandisi Enock Kayani akifafanua jambo kwa timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya Kichina ya Ujenzi (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) wakati walipotembelea eneo la Mradi  katika Kijiji cha Burugo  Halmashauri ya Wilaya Bukoba Mkoani Kagera.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Enock Kayani amesema Mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba Mwaka huu mara baada ya Kampuni hiyo kufanya maboresho yaliyotolewa na Wizara katika michoro yao na kwamba mradi mzima utagharimu fedha za Kitanzania takribani bilioni 22 na utafanyika kwa awamu mbili.
Ujumbe wa Timu ya Wataalam kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Kichina ilipotembelea  shule ya Sekondari ya wavulana Ihungo inayojengwa upya na Serikali mara baada ya kuharibiwa vibaya na tetemekeo la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016. Kampuni hiyo ilitembelea shule hiyo kwa lengo la kujifunza  na kuona aina ya ujenzi wa Miundombinu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Ijumaa, 6 Aprili 2018

DK. SEMAKAFU AZUNGUMZIA HAKI ZA MTOTO


Serikali ya awamu ya Tano  imesema katika kulinda haki za mtoto imedhamiria kujenga shule za Elimu Jumuishi na zile za  wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika kila mkoa.

Kauli hiyo imetolewa na  Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave maria Semakafu jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa wadau unaojadili haki za mtoto.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave maria Semakafu akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau kuhusu haki za mtoto, mkutano ambao umefanyika jijini Dar es salaam.

Dk. Semakafu amesema lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wapata Elimu bila vikwazo vya aina yoyote kwani Elimu ni msingi wa Maenedeleo.

Amesema katika kutekeleza hilo tayari Wizara hiyo inajenga shule ya mfano kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika chuo cha Ualimu Patandi kilichopo mkoani Arusha, ambapo shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wa shule ya msingi mpaka Sekondari.
Wageni waalikwa katika meza kuu wakifuatilia majadiliano kupitia jukwaa la kutetea haki za mtoto.

Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wenye umri wa kwenda shule bila kuangalia changamoto za kimaumbele walizonazo watoto wao kwa kuwa tayari Serikali imewekeza katika eneo hilo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano unaojadili haki za mtoto wakisikiliza kwa makani hotuba ya Naibu katibu Mkuu Dk. Semakafu (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano huo jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa UNICEF katika masuala ya Elimu nchini Tanzania Cecilia Baldeh amesema tayari Tanzania imekwisha piga hatua katika kulinda na kutetea haki za mtoto ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda kwa kuwa Elimu msingi hivi sasa inatolewa bure.
Wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimatifa la nchini Sweden, SIDA wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu kabla ya kufungua mkutano wa wadau wa ndani na nje ya nchi unaojadili haki za mtoto.





Jumatano, 4 Aprili 2018

Waziri Ndalichako: Kila jambo linautaratibu wake katika kulitekeza


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Profesa Joyce Ndalichako amelitaka shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa Shule nchini –TAMONGSCO kuwa na mtazamo chanya wanapotekekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuelewa kuwa kila Jambo linautaratibu wake katika kulitekeleza.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo ambapo amesisitiza kuwa Elimu ni kitu muhimu na hakiwezi kuendeshwa bila kufuata utaratibu, kusisitiza kuwa hata uendeshaji wa shule una taratibu zake.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa  ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa shule (TAMONGSCO) uliofanyika Mjini Dodoma .
Profesa Ndalichako aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali haiwezi kuweka vikwazo na vizuizi kwa wadau wake wa Elimu, kwa kuwa lengo ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa kwa manufaa ya Taifa.


“Hata siku moja Serikali haiwezi kuweka vikwazo na vizuizi kwa wadau ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono  juhudi zinazofanywa na serikali, Pia Serikali inatambua thamani na mchango unaotolewa na sekta binafsi katika Elimu,
 “Hivyo sioni kuwa  ni sahihi kwenu nyinyi TAMONGSCO kuja na kauli mbiu inayosema kuwa  “ Kwa nini vikwazo na vizuizi katika shule na Taasisi zisizo za Serikali,”alisema Waziri Ndalichako.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamilki wa Shule (TAMONGSCO) wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ambaye hayupo pichani wakati akifungua Mkutano huo.   

Waziri Ndalichako pia amewataka Mameneja na Wamiliki hao wa shule kuwa wazalendo kwa kutoa kipaumbele katika kuajiri walimu wa Kitanzania, kabla ya kufikiria wageni.

Amesema ili kuunga mkono kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda ni vyema wawekezaji wakawekeza zaidi kwenye eneo la ufundi stadi, ikiwa ni pamoja na mafunzo yanayotolewa kuendana na soko la ajira.

Kwa upande wao TAMONGSCO wameeleza kuwa lengo la mkutano wao ni kujadiliana kwa pamoja mafanikio na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya Elimu ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa Shule (TAMONGSCO) William Magero akikabidhi risala kwa Mgeni Rasmi katika mkutano Mkuu wa shirikisho hilo  uliofanyika Mjini Dodoma

Jumanne, 3 Aprili 2018

Dk. Semakafu afanya mazungumzo na Kampuni ya Kichina itakayosimamia ujenzi wa VETA, Mkoani Kagera


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) ambayo inatarajia kusimamia ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA cha Mkoa wa KAGERA.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo UDOM mkoani Dodoma ambapo kwa pamoja wamejadiliana hatua za awali za Ujenzi wa chuo hicho na kuwa tayari kampuni hiyo imekwisha andaa michoro ya namna chuo hicho kitakavyokuwa huku wakisisitiza kuwa ujenzi huo utafanyika kwa awamu mbili.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akifanya majadiliano kuhusu ujenzi wa VETA mkoani KAGERA
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu Msaidizi wa kamapuni hiyo Fang Kefang amemweleza Dk. Semakafu kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo itachukua miezi 18 na majengo yatakayojengwa yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi mia nne (400).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza na Meneja Mkuu Msaidizi wa Idara ya Usanifu Majengo wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) Fang Kefeng, Kampuni inayotarajiwa kusimamia ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Stadi, VETA cha Mkoa wa Kagera.



Jumanne, 27 Machi 2018

Wizara ya Elimu yawasilisha Taarifa ya Utekelezaji, Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2018/19 kwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 na Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2018/19 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika leo katika ofisi za Bunge zilizopo Mkoani Dodoma ambapo wajumbe wa Kamati hiyo wamepata fursa ya kupitia na kujadili Fungu 46. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Pro.Joyce Ndalichako  akifafanua jambo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji  2017/18 na Makadirio ya Bajeti kwa Mwaka 2018/19 kwenye Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.


Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Juma Nkamia akisitiza jambo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji na Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19 Mkoani Dodoma.

Wajumbe wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji na Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19.