JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA
TEKNOLOJIA
Anuani
ya simu “ELIMU”
Simu:
026 296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti:
www.moe.go.tz
|
|
Chuo cha Masomo ya
Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L.
P. 10,
40479
DODOMA.
|
TAARIFA KWA UMMA
KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BODI
YA KITAALAMU YA WALIMU TANZANIA
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agosti 21, 2018 imewasilisha
maelezo kuhusu Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania katika
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.
Muswada
wa Sheria hii unalenga kuanzisha Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania itakayosimamia
utaalamu wa ualimu nchini kwa walimu
wote walio katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi kuanzia walimu ngazi ya
Astashahada, Stashahada na Shahada.
Pamoja
na mambo mengine, Bodi itakayoundwa kwa Sheria hiyo: itasajili, itaweka viwango
vya ubora wa ualimu, itasimamia maadili na miiko ya ualimu ya kitaalamu, itafanya
tafiti kuhusu masuala ya utaalam wa ualimu na kusimamia maendeleo ya utaalamu wa
ualimu kwa ujumla.
Uanzishwaji
wa Bodi hiyo ni utekelzaji wa Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohimiza Serikali kuhuisha Mfumo na
Muundo wa Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Sekta ya Elimu ili uwe na tija na
uwajibikaji, na kuhakikisha kuwa maadili na haiba ya walimu yamezingatiwa
katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Inatarajiwa kwamba,
baada ya Sheria inayopendekezwa kutungwa na kutekelezwa ipasavyo, matokeo
yafuatayo kupatikana:
a) Walimu wote nchini kutambuliwa na kusajiliwa na chombo cha kitaalamu,
hivyo kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kushughulikia walimu watakao kwenda kinyume
na maadili ya utaalamu wa ualimu.
b) Kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi, uthibiti na uendelezaji wa utaalamu wa
ualimu.
c) Kulindwa kwa hadhi ya taaluma na utaalamu wa ualimu kwa kuzuia watu
wasiokidhi vigezo na viwango stahiki kufanya kazi ya ualimu.
d)Walimu waliopo katika utumishi wa ualimu kuwa na sifa kulingana na
matakwa ya Sheria inayopendekezwa, na hivyo jamii kupata elimu yenye viwango
stahiki.
Muswada tajwa
unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika Mkutano wa Kumi na Mbili
(12) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kuanza Septemba 4,
2018.
Wizara inawakaribisha wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua zote za
utungwaji wa Sheria hii ili kuweza kupata Sheria bora kwa maslahi mapana ya
walimu na nchi kwa ujumla.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
21/8/2018