Jumatano, 6 Februari 2019

KITENGO CHA MANUNUZI WIZARA YA ELIMU CHATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA SHERIA NA KANUNI ILI KUEPUKA HOJA ZA MKAGUZI MKUU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amekitaka Kitengo cha Manunuzi na Ugavi cha Wizara hiyo kuhakikisha kinafanya kazi zake kwa kufuata sheria na kanuni za manunuzi ili kukwepa hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikiripotiwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali   (CAG).

Prof. Mdoe ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati wa  ufunguzi wa kikao kazi kinachowahusisha wajumbe wa bodi ya manunuzi, Idara ya   manunuzi , kitengo cha ukaguzi wa ndani  na kitengo Cha sheria kutoka Wizara hiyo  lengo likiwa ni kuimarisha Kitengo cha manunuzi kuondokana na hoja za wakaguzi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe na Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na  Ugavi Hirtudice Jisenge wakifuatilia mada inayotolewa wakati wa Kikao Kazi cha wajumbe wa bodi ya manunuzi, maafisa manunuzi, kitengo Cha wakaguzi wa ndani na kitengo Cha Sheria cha kuwajengea uwezo kuhusu kanuni na sheria za manunuzi.


Naibu Katibu Mkuu huyo amewaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa Kitengo hicho kimekuwa na shughuli za manunuzi ambazo zinatumia kiasi kikubwa cha fedha za serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya vyuo na shule, hivyo ni muhimu kuimarisha shughuli za manunuzi ili kuokoa fedha ambazo zinaweza kupotea kwa kutofuatwa kwa taratibu.

"Wizara imekuwa na miradi mbalimbali ambayo inachukuakaribu asilimia 75 ya bajeti ya Wizara, hivyo mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutoa maamuzi sahihi manunuzi, pia  kuwakumbusha wajibu wao wa kufuata sheria na kanuni za manunuzi,”amesema Profesa Mdoe.
Washiriki wa kikao kazi Cha mafunzo ya Sheria za manunuzi wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi. Kikao kazi hicho kinafanyika mkoani Morogoro.

Akizungumzia umuhimu wa kikao kazi hicho,  Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi  wa Wizara hiyo Hirtudice Jisenge amesema mafunzo hayo yatawezesha Kitengo hicho kujipanga na  kufanya kazi kwa ufanisi.

Jumatatu, 4 Februari 2019

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI WATUMISHI 6 CHUO CHA UALIMU PATANDI.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kuwasimamisha kazi watumishi 6 wa Chuo cha Ualimu Patandi kutokana na kushindwa kusimamia vyema ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa Wilayani Arumeru mkoani ARUSHA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ave Maria Semakafu na watendaji wengine wakikagua hali ya ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa katika Chuo Cha Ualimu Patandi mkoani ARUSHA.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo baada ya kukagua hali ya ujenzi unaoendelea wa vyumba vya madarasa, jengo la Utawala, na bwalo la chakula na kisha kuwa na kikao cha pamoja na watendaji wa Chuo hicho kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo yameripotiwa na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Wizara hiyo baada ya kufanyika ukaguzi wa mradi huo wa ujenzi.


Mkuu wa Wilaya ya Arumeru akimuonesha Waziri wa Elimu Prof. Ndalichako hatua za ujenzi wa shule ya wanafunzi wenye mahitaji Maalumu inayojengwa Patandi, shule hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 640.

Kufuatia hali hiyo, Waziri aliagiza kusimamiashwa kazi kwa  Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Issac Myovela, Afisa manunuzi Charles Njarabi, Mhasibu Rose Kijaka, M/Kiti wa kamati ya  mapokezi Peter Mosha na  Msimamizi wa ujenzi huo Israel Mayage.

Wengine ni aliyekuwa Afisa manunuzi wa Chuo hicho Henry Matei ambaye alihamishiwa Chuo cha Ualimu Monduli na kuwa Waziri ameelekeza arudishwe chuoni hapo na asimamishwe kazi mara moja.


Muonekano wa Jengo la Utawala la Shule ya Wanafunzi wenye mahitaji maalumu inayojengwa katika Chuo cha Ualimu Patandi.

Pia Waziri amemuagiza Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo kumpunguzia majukumu ya kazi Mkuu wa Chuo cha Patandi Lyana Mbaji kutokana na kuwa ni mgonjwa na badala yake ateuliwe Mkuu mwingine aweze kuendelea na majukumu katika Chuo hicho.

Mpaka sasa tayari Wizara imekwishatoa kiasi cha shilingi Bilioni 2.3, mradi utakapokamika kiasi ha sh. 2.56 zitakuwa zimetumika.
Muonekano wa Bwalo la Wanafunzi wenye mahitaji maalumu linalojengwa katika Shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Chuo cha Ualimu Patandi, Arumeru mkoani Arusha.

DKT. AKWILAPO AMEWATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA KUZNGATIA KANUNI, TARATIBU NA SHERIA ZA KAZI


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za kazi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa pamoja na watumishi wa Wizara hiyo wenye lengo la kupitia utendaji kazi wa wizara kwa mwaka 2018 na kuweka malengo ya utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2019.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo (hawapo pichani), wakati akifungua mkutano wa pamoja uliofanyika Jijini Dodoma leo, ambao amewataka watumishi kufuata kanuni, taratibu na sheria za kazi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao. 


Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  kutoka  Idara na Vitengo wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa mkutano wa pamoja wa Watumishi wa Wizara hiyo, mkutano huo umefanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu huyo pia amewataka watendaji wa Wizara hiyo kuendelea kuwahudumia wateja kwa lugha nzuri na kuhakikisha huduma zinatolewa katika muda muafaka kwa lengo la kuepusha malalamiko.

“Nichukue fursa hii kupitia mkutano wa wafanyakazi wote kuwataka kutekeleza majukumu yenu kwa kufuata taratibu na sheria za kazi pamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili nchi iweze kufikia malengo ambayo imejiwekea. Kila mmoja atomize wajibu wake katika eneo lake naamini kwa kufanya hivyo tutafanikiwa,” alisisitiza Dkt. Akwilapo.

Watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Makao Makuu) wakiwa katika Mkutano wa pamoja ambapo Katibu Mkuu ameelekeza watumishi kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja na zitolewe katika muda muafaka.

Mkutano   wa pamoja wa Wafanyakazi wa Wizara hiyo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu ambayo Wizara inakuwa imejiwekea.

Mkutano wa pamoja wa Viongozi na watumishi wa Wizara wenye lengo la kupitia utendaji kazi wa Wizara kwa mwaka 2018 na kuweka malengo ya utekelezaji kwa mwaka 2019.

Jumatano, 30 Januari 2019

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WAKURUGENZI KUACHA KULALAMIKA NA BADALA YAKE WATUMIE VIZURI FEDHA ZINAZOTENGWA KWA AJILI YA SEKTA YA ELIMU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka  Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuacha kulalamika kuhusu miundombinu ya shule wakati wanashindwa kutumia vyema fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Elimu.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu utekelezaji wa Programu ya lipa kukingana na Matokeo katika sekta ya Elimu ambapo amewataka watendaji wa halmashauri kuacha kufanya matumizi tofauti na maelekezo yanayotolewa na kama upo ulazima wa kubadili matumizi halmashauri zinapaswa kuomba kibali cha kubadili matumizi na hawatatakiwa kuanza matumizi kabla ya idhini kutolewa.

“Mpango huu wa lipa kulingana na Matokeo unekuwa na mafanikio makubwa katika kipindi Cha kuanzia mwaka 2014/2015 hadi 2017/2018 halmashauri zimekuwa  zikifanya vizuri katika utekelezaji wa vigezo na hivyo kupata ongezeko la fedha kila mwaka kutoka Shilingi bilioni 15.53 (2014/2015) hadi kufikia shilingi bilioni 50 kwa mwaka ( 207/1018),”alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu wa mikoa, maafisa Elimu msingi na Sekondari na  Wathibiti Ubora wa Shule (hawapo pichani),wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu utekelezaji wa Program ya Lipa Kulingana na Matokeo katika sekta ya Elimu. Mkutano huo umehusisha watendaji wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga.

Pia Waziri Ndalichako amewataka Wakurugenzi, Maafisa Elimu na Wathibiti ubora wa shule kuimarisha mfumo wa menejimenti na upatikanaji wa taarifa /Takwimu za Elimu na kuhakikisha kunakuwa na usawazishaji wa ikama ya walimu ndani ya halmashauri.
Watendaji katika sekta ya Elimu wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu utekelezaji  wa Program ya Lipa Kulingana na Matokeo katika sekta ya Elimu. Amewataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa mipango na weledi.

Lengo la programu ya lipa kulingana na matokeo ni kuinua ubora wa Elimu nchini na kuwa fedha kupitia programu hii hutolewa kutokana na kukidhi vigezo vilivyokubalika na kufanyiwa uhakiki ili kuthibitisha kuwa vimetekelezwa.

Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyija katika mikoa yote hapa nchini.
Mratibu wa Mafunzo Elekezi ya EP4R, Lawarence Sanga akitoa maelezo kwa Waziri Ndalichako kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo kwa watendaji katika kusimamia vyema fedha za miradi inayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

WAZIRI NDALICHAKO ASEMA CHUO CHA UFUNDI STADI MKOANI KAGERA KUANZA KUJENGWA


Serikali imekamilisha miundombinu yote muhimu ikiwemo Maji, umeme na barabara kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi VETA mkoani Kagera.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako baada ya kuzindua chanzo cha Maji ambacho kitatumika kwa ajili ya kujenga VETA hiyo katika kijiji cha Burugo, Kwenye halmashauri ya Bukoba.

“Dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuwa nchi ya uchumi wa kati hadi ifikapo mwaka 2025 ili kutimiza malengo hayo ndiyo serikali imewekeza zaidi katika kujenga vyuo vya Ufundi stadi ili kuwa na wataalamu wa kati na wa kutosha watakaotumika kwenye viwanda hapa nchini,” alisisitiza Waziri Ndalichako.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua chanzo cha maji kitakachotumika kujenga chuo cha Ufundi stadi, VETA mkoani Kagera na kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza muda wowote baada ya serikali kukamilisha miundombinu inaayohitajika kama vile maji, umeme na barabarana.

Awali akipokea taarifa ya mkoa huo kuhusu sekta ya Elimu, Waziri Ndalichako ameonesha kutoridhishwa na hatua za ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi mkoani humo na kuzitaka mamlaka husika kutafuta ufumbuzi ili kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi.

Waziri Ndalichako pia ametembelea na kukagua ujenzi unaoendelea wa Chuo cha Ufundi Stadi Karagwe ambapo amemtaka Mkandarasi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika katika muda uliopangwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa chuo cha Ufundi stadi VETA, (KDVTC) Wilayani Karagwe mkoani Kagera ambapo waziri amemuelekeza mkandarasi kukamilisha ujenzi katika muda uliopangwa.


Waziri Ndalichako pia alitembelea Shule ya Bukoba Sekondari ambayo paa za shule hiyo ziliezuliwa kufuatia mvua kubwa Iliyoambatana na upepo na hivyo kulazimika wnafunzi wa shule hiyo kuhamishiwa katika shule ya sekondari Ihungo na wengine katika shule ya Sekondari Omumwani.

Wakala wa majengo ambaye ndiyo Mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Karagwe,  Kilichopo Wilayani Karagwe akijadiliana Jambo na Waziri Ndalichako wakati Waziri akikagua ujenzi wa chuo hicho.

WAZIRI NDALICHAKO ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA CHUO CHA VETA WILAYANI CHATO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako leo ameendelea na ziara yake mkoani Geita ambapo ametembelea mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA kinachojengwa Wilayani Chato mkoani humo na kusema kuwa ameridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Chuo hicho Waziri amesema  upo upungufu  wa vyuo vya kutolea mafunzo ya Ufundi na tayari serikali imeendelea kujenga ili kuhakikisha dhamira ya kuwa nchi ya viwanda inafikiwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Udundi Stadi cha VETA, Wilayani Chato mkoani Geita, akiwa katika ukaguzi huo waziri alisema ameridhishwa na hatua ya ujenzi uliofikiwa.

Waziri Ndalichako ameendelea kuitaka Idara ya manunuzi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inafanya uchaguzi sahihi wa mkandarasi na kuwa hilo ndiyo suluhisho la kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati.

 “Nitumie fursa hii kuzielekeza halmashauri zote nchini kuendelea kukamilisha  majengo na majengo yakishakamilika  basi Wizara tutanunua vifaa kupitia mradi wa kukuza ujuzi na kazi (ESPJ) lengo la serikali  ni kuendeleza ujuzi ili kupata wataalamu wa kutosha,” alisema Prof. Ndalichako.
Muonekano wa moja ya jengo la chuo cha Ufundi Stadi VETA, Wilayani Chato mkoani Geita.

Akiwa Wilayani Chato, Waziri Ndalichako alizungumza na wanafunzi wa kidato cha tano na sita wa shule ya sekondari  ya wasichana ya Jikomboe ambapo ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. Milioni mia mbili kwa ajili ya kujenga bwalo, chumba cha darasa na kumalizia uzio wa shule hiyo.

 Waziri Ndalichako kesho ataendelea na ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi ya vyuo vya Ufundi stadi mkoani Kagera.
Muonekano wa jengo lingine katika mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA, Wilayani Chato mkoani Geita.

WAZIRI NDALICHAKO AITAKA TAKUKURU KUCHUNGUZA MRADI WA UJENZI VETA YA MKOA GEITA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mchakato wa upatikanaji wa zabuni ya ujenzi wa Mradi wa Chuo Cha Ufundi stadi VETA mkoani Geita unaotekelezwa na Kampuni ya ukandarasi inayojulikama kama SkyWard.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA mkoani Geita wakati wa ziara yake ya mkoani humo.

Waziri huyo amesema hajaridhishwa na ujenzi wa mradi huo na kuwa hadi sasa tayari ni miezi mitano  na kwa mujibu wa mkataba bado miezi sita mradi ukabidhiwe, lakini inavyoonekana ni kuwa kampuni hiyo tayari ilishaonesha kushindwa kazi ambayo walishapewa ya ujenzi wa Chuo Cha Ualimu Ndala.

“Mkandarasi hii Serikali siyo ya kuichezea, mwaka mzima sasa bado mko asilimia ambazo haziridhishi pia hakuna kasi ya majengo na hakuna vibarua wanaoendelea na kazi, mnadeni Chuo cha ualimu Ndala, na hapa tena  kwenye ujenzi wa Chuo cha VETA Geita kuna tatizo na hata mazingira ya kumpa huyu mkandarasi kazi, niwaonye watu wa Idara ya manunuzi pale Wizarani kuacha kutoa kazi kwa watu wasiokuwa na uwezo,” anasema Waziri Ndalichako,
Muonekano wa moja ya jengo katika mradi wa ujezni wa chuo cha Ufundi Stadi Mkoani Geita, ambapo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemtaka mkandarasi kukamilisha ujenzi huo katika muda uliopangwa na si vinginevyo.

Waziri huyo yuko mkoani Geita kwa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi wa vyuo vya Ufundi stadi vya Geita na Chato.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Geita wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi kinachojengwa mkoani humo