Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Mh. Prof. Joyce Ndalichako amesema Wizara yake iko tayari kusaidia
kutafuta rasilimali kwa ajili ya
kuanzisha kituo cha kuatamia Ubunifu na Biashara “Innovation and Business
Incubation Centre “ cha Chuo Kikuu Mzumbe, ambacho kitatoa fursa kwa wanafunzi
wanaosoma katika Chuo hicho na Vyuo vingine na vijana wengine wenye mawazo ya
kiubunifu, ujasiriamali na biashara, kuyaboresha mawazo na shughuli zao za
kiubunifu ili ziweze kuwa biashara kamili.
Waziri Ndalichako amesema hayo katika
kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyofanyika katika
Kampasi yake Kuu Morogoro ambapo amepongeza hatua hiyo ya kuanzishwa kwa kambi
hiyo ambayo ni mara ya tatu inafanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, huku
akisema utaratibu huo ni tafsiri sahihi na kwa vitendo ya agenda ya Kitaifa ya
kujenga Uchumi wa Viwanda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiangalia bidhaa zilizotengenezwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo hicho iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro
“Nimefurahi sana leo kuona bidhaa na ubunifu
wa hali ya juu hapa na kusikia kuwa Kambi hii imeendelea kuvutia watu wengi,
wakiwemo wanafunzi, baadhi ya wafanyakazi na watu wengine kutoka jamii
zinazotuzunguka, utaratibu huu utakuwa na faida ya muda mrefu kwa Chuo kwani
wahitimu wenu watakuwa wameiva kinadharia na kivitendo, na wenye uwezo wa
kujiajiri na kutengeneza ajira”.
Ndalichako amevitaka vyuo vingine kuiga mfano huu
ambao unatoa fursa ya kukitangaza Chuo ambapo watanzania wataweza kujionea
namna ambavyo fani mnazofundisha kama Uongozi wa Biashara, Ujasirimali, Uchumi
na Mipango, TEHAMA, na zingine zinavyotayarisha wahitimu ambao wana mawazo ya
kibunifu na ujasiriamali na mtazamo wa kibiashara.
Ndalichako amewataka Chuo Kikuu Mzumbe
kuhahakisha kupitia kituo hicho atamizi kinawezesha wabunifu wao kushiriki
katika mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU), kwa
lengo la kuhamasisha ubunifu nchini yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu Sayansi
na Teknolojia.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akionyesha kitabu kilichoandikwa na Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe mara baada ya kkizindua wakati wa kilele cha kambi ya ujasiriamali ya Chuo hicho iliyofanyika katika Kampasi yake Kuu Morogoro
Akizungumza katika kilele hicho Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka amesema kambi hiyo inashirikisha wanafunzi
wa Mzumbe na wengine, wahitimu wa Mzumbe ambao ni wajasiriamali. Ameongezea pia
kuwa kupitia kambi hiyo wanafunzi wenye mawazo ya kibiashara pia hukutanishwa
na wafanyabiashara walibobea na ili kupata uzoefu. Kusiluka ameahidi kusimamia uanzishwaji wa
haraka wa kituo atamizi kwani kitasaidia kukuza mawazo ya kibunifu kuwa
biashara kubwa nchini zitakazo changia pato la Taifa.
Nae mzungumzaji Mkuu wa kambi ya Mwaka
2019. Ndugu Ahmed Lussasi ambae ni mhitimu wa Chuo kikuu Mzumbe na Mwazilishi mwenza wa kampuni ya MAXOM
AFRICA, kampuni inayofanya vizuri katika biashara, amesema anapongeza wazo la
kituo atamizi na ameiomba Serikali kulipa kipaumbele , kwani biashara yao
ilianza kwa kulelewa katika kituo atamizi na hatimae kukua. Lusassi kama mmoja wa wahitimu amekitaka Chuo
kuwa na mfumo mzuri wa kushirikisha wahitimu wake katika masuala mbalimbali ya
maendeleo ya Chuo hicho.
Katika kambi hiyo Ndalichako amezindua
bidhaa mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi wabunifu na wajasiriamli katika
chuo hicho, ikiwa ni pamoja na kitabu kilichoandikwa na mwanafunzi wa Chuo
hicho. Kwa mwaka 2019 wanafunzi 48 wameandikisha mawazo yao ya kibunifu ili
yaweze kuboreshwa.