Alhamisi, 23 Agosti 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

    Anuani ya simu “ELIMU”
   Simu: 026  296 35 33
   Baruapepe:info@moe.go.tz
   Tovuti: www.moe.go.tz
  



  
     Chuo cha Masomo ya 
     Biashara na Sheria,
     Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
     S. L. P. 10,
     40479 DODOMA.           

   
TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BODI YA KITAALAMU YA WALIMU TANZANIA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agosti 21, 2018 imewasilisha maelezo kuhusu Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma.
Muswada wa Sheria hii unalenga kuanzisha Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania itakayosimamia utaalamu wa ualimu nchini kwa walimu wote walio katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi kuanzia walimu ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada.

Pamoja na mambo mengine, Bodi itakayoundwa kwa Sheria hiyo: itasajili, itaweka viwango vya ubora wa ualimu, itasimamia maadili na miiko ya ualimu ya kitaalamu, itafanya tafiti kuhusu masuala ya utaalam wa ualimu na kusimamia maendeleo ya utaalamu wa ualimu kwa ujumla.

Uanzishwaji wa Bodi hiyo ni utekelzaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayohimiza Serikali kuhuisha Mfumo na Muundo wa Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Sekta ya Elimu ili uwe na tija na uwajibikaji, na kuhakikisha kuwa maadili na haiba ya walimu yamezingatiwa katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Inatarajiwa kwamba, baada ya Sheria inayopendekezwa kutungwa na kutekelezwa ipasavyo, matokeo yafuatayo kupatikana:

a) Walimu wote nchini kutambuliwa na kusajiliwa na chombo cha kitaalamu, hivyo kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kushughulikia walimu watakao kwenda kinyume na maadili ya utaalamu wa ualimu.
b) Kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi, uthibiti na uendelezaji wa utaalamu wa ualimu.
c)  Kulindwa kwa hadhi ya taaluma na utaalamu wa ualimu kwa kuzuia watu wasiokidhi vigezo na viwango stahiki kufanya kazi ya ualimu.
d)Walimu waliopo katika utumishi wa ualimu kuwa na sifa kulingana na matakwa ya Sheria inayopendekezwa, na hivyo jamii kupata elimu yenye viwango stahiki.

Muswada tajwa unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu katika Mkutano wa Kumi na Mbili (12) wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotarajiwa kuanza Septemba 4, 2018.  
Wizara inawakaribisha wananchi kushiriki kikamilifu katika hatua zote za utungwaji wa Sheria hii ili kuweza kupata Sheria bora kwa maslahi mapana ya walimu na nchi kwa ujumla.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
21/8/2018





Jumanne, 21 Agosti 2018

MAPENDEKEZO YA MUSWADA WA SHERIA YA BODI YA KITAALAMU YA WALIMU YAWASILISHWA KWENYE KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Akiwasilisha mapendekezo hayo Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amesema Bodi hiyo itasimamia usajili, weledi na maadili ya kitaalamu ya walimu katika sekta ya umma na binafsi.

Naibu Waziri amesema kupitia bodi hiyo Pia itainua  hadhi ya taaluma ya ualimu kwa kusajili walimu wote kulingana na viwango vya ubora wa ualimu na kuwapa leseni ya kufundisha katika ngazi stahiki.

 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiwasilisha Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma


Pia kupitia bodi hiyo ya kitaalamu itakuwa na jukumu la kuimarisha utaalamu wa walimu kwa kuchochea ari ya kujiendeleza kitaalamu miongoni mwa walimu na kuongeza fursa  za ajira katika soko la ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema utaalamu wa ualimu hapa nchini umekuwa ukisimamiwa na vyombo mbalimbali ambavyo vililenga kwenye ajira, maslahi ya walimu na maadili ya walimu kiutumishi huku masuala ya usimamizi na maendeleo ya utaalamu wa ualimu kutokuwa na sheria na chombo mahususi cha kuyasimamia. 

Amesema  kuundwa kwa Bodi mahsusi ya kusimamia Utaalamu wa Walimu ni suala la msingi katika kuinua ubora wa Elimu nchini na suala hili limezingatiwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotamka bayana kuwa Serikali itahuisha Mfumo na Muundo wa Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji katika Sekta ya Elimu ili uwe na tija na uwajibikaji.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiwasilisha Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Jijini Dodoma

Pia Sera hiyo imetamka kuwa Serikali itahakikisha kuwa maadili na haiba ya ualimu na watumishi wengine yanazingatiwa katika ngazi zote za Elimu na mafunzo hivyo kuanzishwa kwake kuna tija katika usimamizi wa Utaalamu wa Ualimu.

Walengwa wa Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania inayopendekezwa itamhusu mtu yeyote aliyefuzu mafunzo ya ualimu katika Chuo cha Ualimu au Chuo Kikuu kinachotambuliwa na mamlaka husika katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada, Shahada ya Uzamili na  Uzamivu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiwa na Viongozi Wakuu wa Wizara, Wakurugenzi na watumishi wengine wa Wizara wakiwasili katika viwanja vya Bunge kwa ajili ya kuwasilisha Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalamu ya Walimu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii 

Jumapili, 19 Agosti 2018

SERIKALI KUTUMIA MBINU ZOTE ZA UFUNDISHAJI KUWEZESHA WATOTO KUJIFUNZA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali itatumia mbinu zote za ufundishaji ili kuwezesha watoto kujifunza kwa ufanisi.

Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ufundishaji wa maudhui yaliyoandaliwa kwa mfumo wa kietroniki ambayo yatatumia Vikaragosi (Cartoon) kufundishia watoto wa madarasa ya chini.

 Waziri Ndalichako amesema njia hii Itasaidia watoto kuelewa kwa  urahisi kwani wapo  watoto wanaoelewa kwa kuona, kushika na kisikiliza.




Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wadau wa Elimu ( Hawapo Pichani)  wakati wa uzinduzi wa ufundishaji wa maudhui yaliyoandaliwa kwa mfumo wa kietroniki ambayo yatatumia Vikaragosi (Cartoon)


"ikumbukwe kwamba hakuna njia bora kuliko nyingine katika kufundisha, wapo watoto  wanaoelewa zaidi kwa kuona, kusilikiza ama Kufanya kwa vitendo hivyo ni muhimu kutumia njia zote ili tusiache mtoto yeyote bila kuelewa" Amesisitiza Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema matumizi ya Vikaragosi yataleta ari kwa watoto kujifunza kwani wakati wa majaribio ya vikaragosi hivyo walionyesha hali ya kutaka kujifunza kwa kutumia.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akionyesha DVD zenye maudhui ya Kietroniki ambazo zitatumika kufandishia madarasa ya chini wakati wa uzinduzi wa ufundishaji wa maudhui yaliyoandaliwa kwa mfumo wa kietroniki ambayo yatatumia Vikaragosi (Cartoon)

Aidha, Waziri wa Elimu amewataka Maafisa Elimu Kata kote nchini kuhakikisha wanafatilia kwa ukaribu ufundishaji kwa kutumia Vikaragosi hivyo pindi  vitakaposambazwa shuleni.

Jumamosi, 18 Agosti 2018

DK. SEMAKAFU AKEMEA VITENDO VYA UNYANYAPAA DHIDI YA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU.

Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu amewataka walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa wanafunzi hao, kwa kuwa taaluma waliyonayo inahitaji upendo na uvumilivu.

Dk. Semakafu ametoa kauli hiyo mkoani Mwanza wakati akizungumza na walimu hao ambao wanashiriki mafunzo maalumu ya siku 10 ya kuchambua mtaala ulioboreshwa wenye lengo la kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili, wasioona na wanafunzi viziwi.
Naibu Katibu Mkuu akizungumza na walimu wanaoshiriki mafunzo ya kuchambua mtaala ulioboreshwa yanayofanyika katika Chuo Cha Ualimu Butimba mkoani Mwanza

Dk. Semakafu amesema pamoja na mambo mengine amewataka walimu kuacha masuala ya vitengo na badala yake walimu wafanye kazi zao kwa weledi, ikiwa ni pamoja na kuwa wanaharakati katika masuala ya Elimu.

“Walimu naomba niwaambie ukweli huko kwenye shule zetu tumeanzisha vitengo ambavyo havina sababu yoyote na tumekuwa hatufanyi kazi zetu kwa weledi, wengine hatufundishi kwa visingizo vya kuwa tunasimamia vitengo, tuache mara moja na badala yake tufundishe watoto wetu kwa weledi,” alisisitiza Dk. Semakafu.
Walimu wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakifuatilia mafunzo ya kuchambua mtaala mpya ulioboreshwa mkoani mwanza.

Katika mafunzo hayo baadhi ya Walimu walitaka kufahamu kuhusu suala la wanafunzi kuishia Darasa la Sita ambapo Dk. Semakafu alieleza kuwa Elimu inaongozwa na Sheria na Sheria yetu ya Elimu Msingi ni miaka Saba hivyo Sheria ya Elimu haijabadilika.


Mafunzo hayo yanashirikisha walimu 132 wanaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kutoka mikoa wa Kagera, Geita, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Rukwa na Tabora.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akikagua vifaa katika maabara ya Baiolojia katika Chuo Cha Ualimu Butimba, mkoani Mwanza

Ijumaa, 17 Agosti 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ARIDHISHWA NA UKARABATI WA CHUO CHA UALIMU NACHINGWEA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ametembelea Chuo Cha Ualimu Nachingwea na kuridhishwa na kiwango cha ukarabati kinachoendelea ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kimetolewa kwa ajili ya ukarabati huo. 

Akizungumza na watumishi katika Chuo hicho Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kwa mwaka 2018 kwa mkoa wa Lindi kushika nafasi ya pili Kitaifa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na Wazazi pamoja na Walimu (hawapo pichani) wa Shule ya Sekondari Nachingwea Mkoani Lindi mara baada ya kufanya ziara shuleni hapo. 

Naibu Waziri pia amewataka walimu kuhakikisha wanasimamia, wanahamasisha na kuelimisha jamii kuachana na  mila na desturi potofu zinazochangia watoto kuacha shule ikiwa ni pamoja na kushiriki katika unyago.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea na kuipongeza Halmashauri kwa kuwa na wazo la kuwa na Shule ya Sekondari ya wasichana Nachingwea na kuwa hiyo itasaidia watoto wa kike kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa na Viongozi mbalimbali wa Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi akikagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara mara baada ya kupokelewa Chuoni hapo.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema wazazi na wadau wana wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyowanyima fursa, ambapo amewataka Walimu kuhakikisha wanasimamia wanafunzi ili waweze kufikia malengo yao.

Naibu Waziri ameahidi kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili na nyumba 2 za walimu ili kupunguza changamoto za shule hiyo.
Muonekano wa Jengo la darasa lililokarabatiwa katika Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameridhishwa na namna ukarabati wa jengo hilo ulivyofanyika.  

Alhamisi, 16 Agosti 2018

DK. SEMAKAFU: WATHIBITI UBORA NA MAAFISA ELIMU FANYENI UFUATILIAJI SHULENI


Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu amewataka Maafisa Elimu na Wathibiti ubora kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kutoa taarifa kwenye Mamlaka zinazohusika ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Dk. Semakafu ametoa kauli hiyo leo Wilaya Magu mkoani Mwanza wakati akishiriki zoezi la ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na washirika wa Maendeleo kuhusu ufundishaji na ujifunzaji AJESR.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semkafu akizungumza na timu ya ufuatiliaji wa Maendeleo ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni (Hawapo Pichani), Wilayani Magu, mkoani Mwanza.

Dk. Semakafu amesema suala la ufuatiliaji kwa viongozi waliopewa Mamlaka ni la lazima kwani itasaidia zaidi kubaini changamoto lakini pia ni sehemu ya uwajibikaji katika kutimiza malengo ya Taifa.

“Viongozi ni lazima tuwajibike katika kushughulikia masuala ya wananchi na siyo kusubiri kiongozi wa juu aje atoe maelekezo ndiyo tuanze kukimbizana, mfano wewe mthibiti ubora wa shule, au Afisa Elimu unakagua shule zako? unatatua changamoto au unasubiri mpaka Mkurugenzi wa Halmashauri atoe maelekezo?” Alisisitiza Dk. Semakafu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Lutengano Mwalwiba ameahidi kuendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizopo katika Halmashauri hiyo ili Taifa liweze kusonga mbele.
Baadhi ya wajumbe wa timu ya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa na washirika wa Maendeleo wakipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Lutengano Mwalwiba, Mkoani Mwanza.

Amesema hakuna jambo ambalo litaweza kuwa mbadala wa Elimu, Elimu ni kila kitu sasa ikivurugwa Elimu Taifa haliwezi kusonga mbele.

“Tukiwa na misingi mizuri ya Elimu lazima Taifa tutafanikiwa, changamoto zipo na ndiyo maana viongozi tupo kama changamoto zisingekuwepo basi hata viongozi tusingekuwepo,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Semakafu akipokelewa katika Kituo Cha Ufundi Ihushi kilichopo Wilayani Magu, mkoani Mwanza

NDALICHAKO AITAKA VETA MAKAO MAKUU KUPELEKA FEDHA KATIKA WILAYA NA MIKOA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako ameigiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) kuhakikisha inapeleka fedha kwa wakati katika ofisi za Kanda na Vyuo vya  Wilaya na Mikoa ilikuharakisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Mamlaka hizo.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani Katavi ambapo amesema VETA kanda, Mikoa na Wilaya zimekuwa na changamoto za kujiendesha kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
Waziri, Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifalishwa skafu na Mwanafunzi wa Chuo cha VETA Mpanda  ikiwa ni ishara ya kumkaribisha katika Chuo hicho. Waziri Ndalichako aliwashauri vijana na wanafunzi kujiunga katika vikundi vya skauti ili kujiepusha na kujiingiza katika makundi hatarishi

Amesema amesikitishwa kuona baadhi ya mitambo katika Chuo cha VETA Mpanda iliyonunuliwa kwa gharama kubwa na Serkali haifanya kazi kwa kukosekana fedha kidogo za ufungaji wa mitambo hiyo katika karakana za chuo hicho .

“Ukiangalia VETA za mikoani na wilayani zinahitaji fedhak kidogo tu ili zipige hatua lakini hazitolewi, naagiza VETA Makao Makuu kuhakikisha katika mipango yenu mhakikishe mnaweka usawa wa upelekaji fedha kwa VETA zote nchini ili nazo ziweze kupiga hatua katika kutoa mafunzo,”amesema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya mitambo katika moja ya karakana za Chuo cha VETA Mpanda alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu katika Mkoa wa Katavi. Waziri ameitaka VETA Makao Makuu kuhakikisha mitambo yote katika Vyuo vya Wilaya na Mikoa inafanya kazi .

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameahidi kutoa cherehani mbili kwa wanafunzi Gift Giles na Benitha William wwenye umri wa miaka kumi na tano ambao wamejiunga katika Chuo cha VETA Mpanda baada ya kutokuchaguliwa kuendeleana masomo ya kidato cha kwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Amos Makala amenuahidi Waziri kuwa atakisimamia Chuo cha VETA Mpanda ili kiweze kuwa na tija kwa wanakatavi.