Jumatatu, 12 Agosti 2019

SERIKALI YA TANZANIA KUIMARISHA TAFITI KWA AJILI YA KUKUZA NISHATI ENDELEVU NA KUIMARISHA TEKNOLOJIA YA MAJI

Serikali imeendelea kuongeza ubora  wa elimu na kukuza ujuzi ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza ajira nchini. Hii  imewezekana kwa kuweka sera, mifumo na miundo mbinu wezeshi kwa watanzania kuweza kupata ujuzi na umahiri unaohitajika katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya mpango wa  maendeleo 2025 na malengo endelevu ya milenia.

Kauli hiyo  imetolewa Jiji Arusha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa tatu wa Kimataifa wa Nishati endelevu na Teknolojia ya maji (International Conference on Energy, Aquatech and Sustainability 2019, ICEAS) )wenye lengo la kujadili changamoto zinazokabili sekta  ya Nishati  hususan kukuza nishati mbadala na Teknolojia ya  Miundombinu ya maji na kuja na mapendekezo ya namna bora ya kutumia rasimali zilizopo katika jamii kukuza sekta hizo. 
 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Nishati endelevu na Teknolojia ya maji (ICEAS) unaofanyika NM-AIST jijini Arusha.
Amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inajenga uchumi wa viwanda ni kuhakikisha kuwa elimu itolewayo inakuwa bora na kuendeleza ujuzi kwa watanzania ili waweze  kuongeza thamani katika mazao kutumia teknolojia ya kisasa, ambapo maji na nishati ni maeneo muhimu katika kutekeleza hili.

"Tunataka kuona  kama ni mkulima anakuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao kwa kutumia Teknolojia za kisasa na hasa kutumia tafiti zilizofanywa,"  alisema Waziri Ndalichako
Baadhi wa wajumbe wa Mkutano wa ICEAS wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jijini Arusha.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameipongeza Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa kuboresha kiwango  cha utafiti katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na programu wanazotoa.

"Mwaka 2017 hapa NM-AIST tumefanya uzinduzi wa vituo vinne vya umahiri vya Sayansi na Teknolojia katika elimu ya juu kwa lengo la kuhakikisha tunaboresha elimu yetu na kunakuwa na wigo mpana wa kufanya tafiti, tunaona sasa mnafanya vizuri na kuendana na moto wa Chuo ambao ni Taaluma kwa jamii na viwanda, na hata maji ya kunywa yanayotumika katika mkutano huu ni moja ya kazi za tafiti zinazofanyika hapa"aliongeza Waziri Ndalichako
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo ya tafiti zilizofanyika kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Mkutano wa ICEAS unaofanyika katika Taasisi ya NM-AIST jijini Arusha.
Waziri Ndalichako kabla ya kutoa hotuba yake ametumia fursa hiyo kutuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ndugu jamaa na marafiki kufuatia vifo vya watanzania vilivyosababishwa na ajali ya moto  jijini Morogoro Agosti 10, 2019. 

Naye Makamu Mkuu wa Chuo katika Taasisi ya Sayansi Teknolojia ya Nelson Mandela ambae pia ni  Mwenyekiti Mwenza wa ICEAS Profesa Emmanuel Luoga amesema mkutano huo umewaleta pamoja wataalamu wa nishati mbadala na endelevu na watafiti kutoka nchi mbalimbali ambapo mada 37 zitawasilishwa  wataalamu kutoka nchi 11 zilizoshiriki mkutano huo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akibadilishana mawazo na mmoja wa wajumbe wa mkutano wa ICEAS Jijini Arusha.
Mada zitakazojadiliwa  zitajikita katika maeneo ya mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji wa  maji, nishati mbadala na endelevu.

Aidha amesema Taasisi anayoingoza itaendelea kushirikiana na taasisi na vyuo vingine kutoka ndani na nje ya nchi kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii pamoja na kuendeleza viwanda.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza na uongozi wa Taasisi ya NM-AIST mara baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufungua Mkutano wa ICEA unaofanyika katika Taasisi hiyo Jijini Arusha.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela na Chuo cha Taifa cha Seoul cha  Korea chini ya uratibu wa Kituo cha Umahiri ambacho kinashughulika na  miundombinu ya maji na Nishati endelevu na Kituo cha umahiri cha ubunifu na Teknolojia ya Nishati na unafanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 12, 2019 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa ICEAS mara baada ya kufungua mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili katika Taasisi ya NM-AIST jijini Arusha.

Jumamosi, 10 Agosti 2019

BILIONI 4.6 KUJENGA NA KUKARABATI CHUO CHA UFUNDI KARAGWE

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.

Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta a elimu wilayani humo.
Ole Nasha amesema serikali imeweka mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha  kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.


“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akisikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.


Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wa wanaosoma katika Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ambapo amewasisitiza kusoma kwa bidii na kuwataka kuthamini mafunzo wanayoyapata kwani muhimu katika kujiletea maendeleo na kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.
Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa kutokukamilika kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo za kimkataba na kuwapelekea kuomba kuongezewa muda wa miezi sita  baada ya muda wa mkataba kuisha Julai 26,2019.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Godwini Kitonka amesema Halmashauri yake inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.
Baadhi ya majengo yanayojengwa katika Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya yaa Karagwe, ambapo serikali kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo katika chuo hicho.
Mwanafunzi Masau Josephat, wameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo, kwani mwanzoni hayakuwa yakiridhisha, huku wakiiomba serikali kuongezea baadhi ya kozi ambazo hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa maarifa na stadi kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.

Alhamisi, 8 Agosti 2019

WIZARA YA ELIMU YAKUTANISHA WADAU WA MAFUNZO YA ELIMU YA UALIMU ILI KUTOA MAONI YA KUBORESHA MTAALA WA ELIMU YA UALIMU


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inakusudia kufanya maboresho ya mtaala wa elimu ya ualimu ili iendane na mitaala mipya ya elimu ya Sekondari na msingi ambayo imeanza kutumika mwaka 2015.

Hayo yamesemwa Jijni Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu ambao wamekutana kwa lengo la kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha usimamizi na maendeleo hususan maboresho ya mtaala  wa elimu ya ualimu.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu kuhusu usimamizi na uendeshaji bora wa Elimu ya Ualimu uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


Dkt.Akwilapo alisema mtaala wa mafunzo ya ualimu uliopo sasa ni wa zamani  akitolea mfano mtaala wa mafunzo ya  ualimu kwa walimu wa diploma ambao ni wa mwaka 2008 huku ngazi ya cheti ukiwa wa mwaka  2009 hivyo kutoendana na mtaala mpya wa elimu msingi ambao unazingatia ufundishaji wa KKK.

“Elimu ni suala la Kitaifa hivyo serikali haiwezi kujifanya haisikii jamii inasema nini ndio maana kikao cha wadau kimeitishwa na pia Waziri wa elimu yupo mbioni kuitisha mkutano wa wadau kwa lengo la kupata maoni ya namna bora ya  kuboresha Elimu,”aliongeza Dkt Akwilapo.

Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka wadau hao kutumia mkutano huo kujadili na kutafakari kwa kina mfumo wa maandalizi ya walimu nchini kwa kuzingatia mada ya Usimamizi na Maendeleo ya Elimu ya Ualimu, Fursa na Changamoto   pamoja na upimaji na tathmini yake.

“Tumieni mkutano huu vizuri na mambo mtayakojadili yajikite katika kuona ni namna gani mnaboresha mahiri zinazohitajika kwa mwalimu, ama mkufunzi, mazingira na miundombinu wezeshi, uongozi na usimamizi wa mafunzo, upimaji na tathmini ya mafunzo pamoja na maendeleo endelevu ya mwalimu,” alisisitiza Dkt Akwilapo.

Wadau wa Elimu ya Ualimu wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau hao uliofanyika jijini Dar es Salaam.


Akizungumza katika Mkutano huo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa  amesema  mkutano huo wa wadau wa  elimu utachochea mabadiliko katika sekta nzima ya elimu kwani ili kufanikiwa katika sekta hiyo ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa wadau wa elimu.
 
“Tumekutana kwa ajili ya kuongelea moyo wa Taifa letu, Elimu ni moyo wa taifa unaposema elimu unapozungumzia elimu ya ualimu katika kuleta mabadiliko ya sekta nzima ya elimu,” aliongeza Dkt Mtahabwa.

Dkt Mtahabwa anasema unaweza kujenga shule nyingi, ukawa na vifaa vya kutosha lakini kama hauna walimu bora ni kazi bure hivyo tunataka walimu wawe na waledi, wawe kioo cha jamii kuanzia uvaaji wake, kutembea, kuongea na namna anaivyoishi shuleni na hata kijijini awe mfano wa kuigwa katika jamii.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu Augusta Lupokela akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau wa Elimu ya Ualimu ambapo amesema matokeo ya Mkutano huo yatasaidia katika maandalizi ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya ualimu.


Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Augusta Lupokela alimweleza Katibu Mkuu kuwa mkutano huo, pamoja na mambo mengine umelenga kujadili masula yanayohusu usimamizi wa mafunzo ya ualimu na kwamba mada zitakazowasilishwa zitahusu usimamizi na maendeleo ya Elimu ya ualimu, fursa zilizopo pamoja na changamoto.

Aliongeza kuwa matokeo ya mkutano huo ni maandalizi ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya ualimu ili kufikia malengo ya serikali ya kutoa elimu bora ya ualimu.

Wadau wa Elimu ya Ualimu wakiwa wameshikana mkono huku wakiimba wimbo wa “solidarity” kuashiria umoja katika utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo mapana ya kutoa elimu iliyo bora.


Nae Mratibu wa mradi wa Elimu kwa Walimu (TESP) Ignasi Chonya amesema kupitia mradi anaousimamia wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu kazini na walimu tarajali kuhusu matumzi ya TEHAMA, ualimu kwa vitendo kwa vyuo vyote vya Serikali na binafsi ili kuwajengea uwezo wa namna ya kufundisha kwa vitendo.

Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu unafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 08, 2019 na  umehusisha wadau kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Taasisi zake, Viongozi na Mameneja wa shule, vyuo vya ualimu kutoka sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wizara ya Elimu.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa mkutano wa wadau wa elimu ya ualimu baada ya kufungua mkutano huo jijini Dar es Salaam.


Jumanne, 6 Agosti 2019

OLE NASHA AAGIZA MKANDARASI WA UKARABATI WA SHULE YA SEKONDARI KULIPWA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha Mkandarasi anayekarabati shule ya sekondari Bukoba ili aweze kuendelea na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyu amelipwa kiasi cha shilingi milioni 32 tu.

“Fedha zilishaletwa zote na wizara shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni 32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa mpaka sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha Mzinga wanapata fedha ambazo wanadai” amesisitiza Ole Nasha.
 
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akikagua baadhi ya majengo ya shule ya Sekondari Bukoba ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kumlipa Mkandarasi ili ukarabati uendelee.


Ole Nasha amesema ukarabati wa shule hiyo unaoendelea umechelewa kukamilika kwani licha ya fedha hizo kupelekwa mapema mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo. Hata hivyo amesema kasi ya ujenzi huo si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.

Aidha, Ole Nasha amewataka watendaji wa manispaa hiyo kufuatilia kwa ukaribu matumizi ya fedha hizo kwani ni nyingi kutumika kwa ukarabati ukilinganisha na fedha zinazotumika katika miradi mingine, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa fedha kubaki na kutumika katika kufanya shughuli nyingine za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

“Nikifananisha fedha ambazo tumetumia kwenye maeneo mengine na miradi mingine mfano miradi ya afya ambao wanatumia bilioni 1.5 kujenga hospitali kubwa kwa kujenga majengo mapya makubwa saba lakini sisi hiyo bilioni 1.4 ambayo inakaribiana na bilioni 1.5 ya afya tunakarabati majengo tu, kuna umuhimu wa kuzisimamia fedha hizi kwa ukaribu," alisema Ole Nasha.

Aidha, Naibu Waziri amesema shule hiyo ina nafasi finyu ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi mia saba waliopo na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo kuwasiliana na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ambao wana eneo karibu na shule hiyo washaurine juu ya uwezekano wa kutoa eneo hilo kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo.
 
Muonekana wa Shule ya Sekondari Bukoba inayofanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 ambapo baadhi ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa na baadae paa kuezuliwa na upepo mkali.

Awali Mkuu wa shule ya Sekondari Bukoba, Raymond Mutakyawa, amemweleza Naibu Waziri kuwa ukarabati wa shule hiyo ulikuwa ufanyike kwa siku sabini tano na ulipaswa kuwa umekamilika mwishoni mwa mwezi wa saba lakini ulisimama kutokana na kukosa fedha za kununua vifaa kwa ajili ya kazi hiyo baada ya mfumo wa malipo kufungwa kabla ya fedha hizo kulipwa kwa mkandarasi.


 
Shule ya Sekondari ya Bukoba inafanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 lililoikumba mkoa wa Kagera ambapo baadhi ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa na baadae paa kuezuliwa na upepo mkali.

Jumapili, 4 Agosti 2019

OLE NASHA: SERIKALI HAITAMVUMILIA MTENDAJI YEYOTE ATAKAYEHUJUMU FEDHA ZA UJENZI WA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SHULE


 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameagiza watendaji  wa idara ya uthibiti ubora wa shule kusimamia kwa makini miradi ya ujenzi wa ofisi za Uthibiti ubora wa shule pamoja na fedha zinazotumwa kwa ajili ya ujenzi huo katika Halmashauri za wilaya mbalimbali nchini.


Naibu Waziri Ole Nasha amesema hayo mkoani Geita wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema serikali haitamvumilia mtumishi yeyote atakayehujumu ama kutumia vibaya fedha hizo zilizotolewa na wizara kwa ajili ya kujenga ofisi hizo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita (Hawapo Pichani) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hizo ambapo ameipongeza Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa ofisi hizo.
Amesema miradi ya ujenzi wa ofisi hizo ni muhimu sana kwa wizara kwani ili kuwa na maendeleo katika sekta ya elimu lazima kuwa na uthibiti ubora wa shule ulio mahiri, wenye uwezo wa kukagua shule na wenye vitendea kazi vya kuwezesha wathibiti ubora wa shule kufanya kazi katika mazingira wezeshi.

“Kama tunataka kuwa na maendeleo katika sekta ya Elimu lazima kuwe na usimamizi thabiti na ndio maana tumechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tumeboresha idara ya uthibiti ubora kwa kuhuisha mfumo kutoka kuwa ukaguzi na kuwa uthibiti kwa maana kwamba unashirikisha kila mtu katika hatua zote,” amesema Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikangua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za wathibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambapo yupo mkoani humo kukagua utekelezaji wa  miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu.
Ole Nasha amesisitiza kuwa haiwezekani kufanya kazi ya uthibiti ubora wa shule kama hakuna ofisi, vitendea kazi ikiwemo magari na ndio maana kila Afisa Elimu wa Kata kwa nchini nzima alipewa pikipiki ya kumwezesha kufanya kazi. Serikali pia ilitoa magari 45 kwa wilaya mbalimbali na sasa halmashauri zipatazo 100 zinajengewa ofisi za uthibiti ubora.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi hizo, Wizara itapeleka vifaa vyote muhimu kwenye ofisi hizo ili kurahisisha kuchakata taarifa zote za elimu kutoka maeneo yote ya nchini kwa lengo la kurahisha huduma za kielimu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiangalia baadhi ya vitabu katika maktaba ya shule ya wasichana ya sekondari Nyankumbu alipofikia  shuleni hapo kukagua  chumba chs kompyuta, waziri Ole Nasha yupo Mkoani Geita kwa ziara ya Kikazi
Aidha, Waziri Ole Nasha amesema ameridhishwa na usimamizi na matumizi ya fedha za ujenzi wa ofisi za uthibiti ubora Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha Mikoa ya Geita, Mwanza na Mara ambayo kwa ujumla inajengewa ofisi 15 zenye thamani zaidi ya bilioni 2.28.

Katika ziara hiyo Waziri Ole Nasha amekagua majengo ya uthibiti ubora wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Halmashauri ya mji wa Geita. Ole Nasha pia amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni mawili na vyoo katika shule ya sekondari Mwatulole ambayo inatarajiwa kuanzisha kidato cha tano hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akisikiliza maelezo ya kuhusu kompyuta kutoka kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwatulole s alipofikia  shuleni hapo kukagua  maendeleo ya ujenzi wa mabweni mawili pamoja na madarasa unaotekelezwa na wizara ya Elimu.
Shule nyingine aliyotembelea ni shule ya sekondari ya Wasichana Nyankumbu ambapo ametembelea chumba cha kompyuta na ameahidi kupeleka kompyuta 50 shuleni hapo ili kuongeza ari ya kujifunza.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ali Kidwaka alimweleza Naibu Waziri kuwa ameshirikiana na watendaji wengine kufanikisha ujenzi ambao uko kwenye hatua ya ukamilishaji na kuahidi kuwa ataendelea kusimamia ili jengo hilo likamilike kwa wakati.
Muonekana wa jengo la ofisi za uthibiti ubora wa shule ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita huku ujenzi ukiendelea. Jengo hili ni moja ya majengo ya ofisi za wathibiti bora kati ya matano yanayoendelea kujengwa katika Mkoa wa Geita.


Jumamosi, 3 Agosti 2019

SERIKALI IMETOA MILIONI 100 KUJENGA BWENI LA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM HALMASHAURI YA MJI GEITA

 Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika halmashauri ya Mji Geita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara mkoani Geita ambapo amesema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalum katika kituo Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.
Ole Nasha amesema serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwajengea fursa na mazingira mazuri ya kusoma watoto wenye mahitaji maalum na ndio maana imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia  pamoja na vitabu ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.

“Kwa miaka mingi jamii nyingi zimekuwa zikiwatenga watoto wenye mahitaji maalim, lakini kwa sasa nashukuru tumeendelea kuwawezesha kupata haki yao ya Elimu kama walivyo watoto wengine na kwamba wanaweza kuwa na changamoto za kimaumbile lakini ubinadamu wao upo palepale” amesema Waziri Ole Nasha.
 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na watoto wenye mahitaji maalum (Hawapo Pichani)  baada ya kukagua ujenzi wa bweni la Kituo cha Watoto wenye mahitaji Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.
Amewataka wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kutokatishwa tamaa na changamoto walizonazo za kimaumbile kwani serikali imewawekea mazingira ya kuwawezesha kufika mbali zaidi katika Elimu na kuwataka kuendelea kutumia fursa hizo za kielimu ili kutengeneza maisha yao ya baadaye.

 
“Wanafunzi, mtu hawezi kujua kipaji chako ni kipi lakini serikali inakupa fursa ya kuonyesha kipaji chako, Mhe Rais ametambua uwezo mkubwa wa watu wenye mahitaji maalum na ndio maana siku hizi tunae Naibu Waziri anayeshughulika na watu wenye mahitaji maalum ambaye naye ana changmoto ya ulemavu,” amesema Naibu Waziri.
 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akicheza na watoto wenye mahitaji maalum katika kituo cha Watoto wenye mahitaji maalum cha shule ya msingi Mbugani, Waziri huyo yupo mkoani Geita kwa ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu

Awali Mwlimu Mkuu wa Shule ya msingi Mbugani Edwicka Ndunguru
  amemweleza Naibu Waziri kuwa  kituo hicho kilijengwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata haki ya kielimu katika mazingira wezeshi na kuwapa fursa wengi zaidi wenye mahitaji maalum wanaoishi mbali na shule zinazotoa elimu maalum kupata elimu.

Amesema mafanikio ya kuwepo kwa vituo vya watoto wenye mahitaji maalum mbali na kuwawezesha kupata haki yao ya kielimu, pia imewasaidia kujifunza ujuzi mbalimbali, jamii imetambua nakuthamini umuhimu wa wanafunzi wenye mahitaji maaluma kupata Elimu na wengine kufanikiwa kupata kazi katika maeneo mbalimbali.
 
Sehemu ya bweni lilojengwa na serikali katika Kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita

“Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapomaliza hapa wanakua na ujuzi katika fani za ushonaji, ufumaji na useremala, fani hizi zimewezesha baadhi kuajiriwa katika maeneo mbalimbali na wengine kujiajiri” amesemu mwalimu Ndunguru.

 
Kituo hicho chenye vitengo vinne vyenye jumla ya wanafunzi 143 ambavyo ni vitengo vya ulemavu wa akili, Viziwi, ulemavu wa viungo na ulemavu wa macho, mbali ya kuhudumia wanafunzi hao wenye uwezo wa kufika shuleni lakini pia vinahudumia watoto 38 wenye ulemavu wa kiwango cha juu ambao hawawezi kufika shuleni.
Ijumaa, 2 Agosti 2019

MAONESHO YA WANASAYANSI WATAFITI WACHANGA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  amesema Serikali inatambua umuhimu wa Sayansi Teknolojia na Ubunifu ktk maendeleo ya taifa letu na hivyo itaendelea kusimamia na kuendeleza wanasayansi wabunifu  nchini.
Amesema hayo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya tisa ya wanasayansi watafiti wachanga nchini yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania, (YST) jijini Dar Es Salaam
Maonesho hayo huwahusisha wanasayansi wanafunzi kutoka shule za sekondari kote nchini , kuonesha tafiti walizofanya kupitia mpango wa YST. 
Ndalichako amewapongeza wanafunzi walioshiriki kwa kuonesha tafiti zilizofanywa kisayansi na ubora na pia kwa kutumia teknolojia katika kubuni mambo mbalimbali  na mifumo inayotoa utatuzi wa  changamoto za jamii yetu. 
Amepongeza walimu wanaoshiriki katika mpango huo kwa kuweza kutoa hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na hisabati na kwa kufundisha vizuri hali ambayo inajionesha kupitia kazi bora za wanafunzi wao.