Jumanne, 31 Oktoba 2017

TEWW yatakiwa kutekeleza  majukumu yake

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Ole Nasha ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kimuundo badala ya kufikiria kufanya miradi ambayo imekuwa ikiwaondoa kwenye mwelekeo wa malengo ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo  ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kuzitambua taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na utendaji wa majukumu yake.
Akiwa katika Taasisi hiyo amesema nchi bado inaihitaji Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na aina ya elimu ambayo inatolewa na taasisi hiyo, hivyo ameitaka taasisi hiyo  kutekeleza majukumu yake iendane na hali halisi ya mazingira ya elimu.
Ole Nasha amesema ukiangalia utekelezaji wa miradi  hiyo inabaki kuitwa elimu ya watu wazima lakini namna inavyoendeshwa haziakisi uhalisia wake na badala yake zinabaki kuwa kama mifumo mingine ya utoaji wa elimu ya mfumo rasmi.

Naibu Waziri Ole Nasha akiwa katika taasisi hiyo amepata fursa ya kutembelea chumba cha Uchapaji vitabu  majarida, Karakana, Maktaba na idara ya Elimu ya masafa na Studio za kuandaa vipindi vya kuelimisha umma vya Elimu ya Watu Wazima.
Aidha, Naibu Waziri ametembelea Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Elimu, Habari, utamaduni  ya UNESCO na kuwataka kuitisha kikao cha wadau wanaohusika na Tume hiyo ili kuzungumzia changamoto za kimfumo na muundo zinazoikabili taasisi hiyo.






Naibu Waziri Ole Nasha atoa maagizo kwa Bodi ya Mikopo na Tume ya Vyuo Vikuu


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amezitaka Tume ya Vyuo Vikuu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhakikisha wanakamilisha taratibu za udahili na utoaji mikopo kwa wakati ili wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu waanze mara moja bila kuchelewa.

Naibu waziri Ole Nasha ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Taasisi hizo ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa ili kujionea utendaji kazi wa taasisi hizo.

Naibu Waziri amesema serikali imeidhinisha takribani shilingi bilioni 427 kwa ajili ya wanafunzi 122,000 wanaoanza na kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.
“lengo la Serikali ni kuona wanafunzi wote wanaanza masomo bila kuchelewa na katika kutekeleza hilo tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 147 kwa Bodi ya Mikopo kwa ajili ya robo ya kwanza ya kuwawezesha wanafunzi wenye sifa na vigezo wanaoanza na wale wanaoendelea masomo yao hivyo hatutegemei kusikia malalamiko yoyote kutoka kwa wanafunzi wanaostahili mikopo hiyo” alisisitiza Ole nasha

Pia ameitaka Bodi kutoa taarifa kwa umma majina yote ya wadaiwa sugu wa mikopo ambao mpaka sasa hawajaonyesha utayari wa kurejesha mikopo hiyo kwani lengo la serikali ni kuona bodi ya mikopo inaanza kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Katika hatua nyingine Mhe. Ole Nasha ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha mfumo unaotumika kudahili wanafunzi  kutochelewesha wanafunzi kupata mikopo kwa wakati ili kuwawezesha kujiunga  na vyuo mapema.

Ole Nasha ameitaka Taasisi hiyo kushirikiana na wanafunzi kwa karibu katika kipindi hiki cha udahili ili kufikia Novemba 2 mwaka huu zoezi hili la udahili liwe limekamilika.




Waziri Ndalichako ashiriki mkutano wa UNESCO, nchini Ufaransa.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni -UNESCO -IRINA BOKOVA amesema Tume hiyo   ina nguvu kwa sababu ya ushirikiano inaoupata kutoka kwa nchi wanachama, hivyo ameziomba  nchi hizo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Bukova ameyasema hayo hii leo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa UNESCO unaohusiha nchi wanachama duniani kote ambapo amesisitiza pia suala la kudumisha amani, upendo miongoni mwa nchi hizo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Balozi wa Tanzani nchini Ufaransa balozi Samweli Shelukindo wameshiriki mkutano huo.


Alhamisi, 19 Oktoba 2017

Mradi wa kuwawezesha watoto wa kitanzania kupata elimu wazinduliwa


Kaimu Mkurugenzi mafunzo ya Ualimu Basiliana Mrimi  amezindua mradi wa shilingi milioni 500 utakaosaidia kuimarisha Ufundishaji na ujifunzaji kwenye Chuo cha Ualimu, Patandi kilichopo mkoani Arusha.

Akizundua Mradi huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mrimi amesema  mradi huo utasaidia Kupima macho watoto wa shule za msingi na kuwapatia vifaa wanafunzi wenye uoni hafifu, Kutoa mafunzo kazini kwa wakufunzi 12 na walimu 4 wa shule za msingi zilizopo kwenye mradi.

Pia mradi huo utasaidia Kusomesha mkufunzi 1 kwa ngazi ya Shahada ya Uzamivu (PhD), Kusomesha wakufunzi 4 kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili (Masters) na kuwa mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania na Norway.


Jumatano, 18 Oktoba 2017

Waziri Ndalichako azindua ufadhili wa wanafunzi unaotolewa na Barclays


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka wanafunzi kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupata taarifa zitakazowasaidia kutekeleza fursa mbalimbali za kujiletea Maendeleo.
Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo  wakati wa uzinduzi wa Twende kazi na Balozi mwanafunzi unaohusu ufadhili wa masomo kwa wanafunzi  23 wa shahada ya kwanza ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kusisitiza kuwa taasisi nyingine ziige mfano huo wa Barclays wa kufadhili wanafunzi.

Pia Barclays imewasaidia vijana 32 Kati ya 200 kuwatafutia ofisi ili kufanya kazi kwa vitendo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuwa tayari kwa kazi.

Uzinduzi huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Sylivia Temu.



Ijumaa, 13 Oktoba 2017

Waziri: Ndalichako: Shule ya nyasi zitabaki kuwa historia

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo amekagua na kufungua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi kilole, Matondoro,  na Kilimani na kuweka jiwe la msingi bweni la wasichana katika shule ya Sekondari Semkiwa  Wilayani Korogwe Mkoani Tanga.

Akizungumza Mara baada ya kukagua utekelezaji wa miradi hiyo Waziri Ndalichako amesema  suala la nchi kuwa na shule au vyumba vya madarasa vya nyasi litabaki kuwa historia kwa kuwa serikali ya awamu ya Tano inahitaji wanafunzi wapate Elimu bora inayoenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu na hicho ndicho kinachofanyika hivi sasa.

Akizindua bweni moja la wasichana katika shule ya Sekondari Semkiwa waziri Ndalichako ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kununulia vitanda na magodoro ili bweni hilo lianze  kutumika mara moja.

Pia amewataka watanzania kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa namna anavyojitoa  katika kuwatumikia Wananchi wanyonge kwa lengo la kuliletea Taifa Maendeleo.

Ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa,na  vyoo umetekelezwa  na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Lipa kulingana na matokeo, (EP4R).




TANGAZO


Jumatano, 11 Oktoba 2017

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi wampokea Mtukufu Agha Khan


Mtukufu Aga khan muda mfupi Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa jijini Dar es Salama na amepokelewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi.



Mtukufu Aga Khan akikagua gwaride lililoandaliwa kwa ajili yake muda mfupi  baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa jijini Dar es salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolonia Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi wakiwa katika picha ya pamoja  na Mtukufu Aga Khan ambaye amewasili leo.




Jumanne, 10 Oktoba 2017

Mradi wa TEHAMA wazinduliwa Mkoani Pwani


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amezindua mradi wenye thamani ya  zaidi ya shilingi bilioni 4 wa ujifunzaji na ufundiashaji wa TEHAMA kwa shule za Sekondari.
Akizindua mradi huo mkoani Pwani hii leo Dkt. Akwilapo amsema Serikali inahitaji kuona mradi huu unakuwa  endelevu na usiishie katika mkoa wa Pwani pekee bali usambae kwa nchi nzima.
Pia amewataka waratibu wa mradi huo - gesci -  kuhakikisha mpango huu unafanikiwa kwa kushirikisha  wadau wote wa Elimu ili mradi  ufanikiwe.
Dkt. Akwilapo amesema TEHAMA ni nyenzo muhimu katika ulimwengu wa mawasiliano, na kwa sasa ndiyo nyenzo kuu ya utoaji na usambazaji wa taarifa kwa umma.
Katibu Mkuu Akwilapo amewataka wale wote wenye miradi au mipango ya namna hiyo wawasiliane na wizara ili miradi yao iweze kuratibiwa na  kutekelezwa kwa taratibu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mradi huo unatekelezwa katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, na Cotedvoire





Jumatatu, 9 Oktoba 2017

VIONGOZI WA WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAAHIDI KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa kitendo cha Rais  John Magufuli kumbakisha kwenye Wizara hiyo ni sawa na kumchagua upya,  hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii.

Waziri Ndalichako amesema hayo wakati akimkaribisha Naibu waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ambaye ameapishwa leo kuitumikia Wizara  hiyo.
 
Wakati akizungunza na Watumishi wa Wizara hiyo Naibu Waziri  Ole Nasha amesema  katika utumishi wake anaamini katika mambo manne ambayo ni uadilifu na uaminifu,  kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ushirikiano ili kutimiza malengo ya Kitaifa.

 Ole Nasha amesema hayo muda mfupi baada ya kupokelwa na watumishi wa Wizara hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kuendeleza Sekta ya Elimu.




Alhamisi, 5 Oktoba 2017

Waziri Ndalichako azindua Bodi ya Wakurugenzi HESLB na Baraza la TET

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknnolojia Prof. Joyce Ndalichako amelitaka  Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania na Bodi ya wakurugenzi ya Bodi ya mikopo ya Wanafunzi  wa elimu ya juu kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za kazi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa bodi hizo ambapo amezitaka pia kuhakiksha zinarudisha hadhi ya Taasisi  za serikali wanazozisimamia katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuweka miongozo ya utendaji kazi na kuhakikisha wanaisimamia miongozo hiyo ili kuleta ufanisi katika kazi.

Ndalichako amezitaka bodi hizo kuhakikisha zinatembea katika ahadi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli za kuhakikisha zinawasaidia wanyonge kupata Elimu bora.

Waziri Ndalichacho amelitaka Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania kuhakikisha vitabu vyote vyenye makosa vinarekebishwa na kwamba bodi ijiridhishe na mfumo na utaratibu utakaotumika katika kuvirekebisha vitabu hivyo.

Baraza hili ambalo litahudumu kwa miaka mine (4) kuanzaia septemba 2017 hadi septemba 2021 limetakiwa pia kusimamia Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma vizuri kwa sababu kumekuwa na upotoshaji kuhusiana na Taasisi lakini pia amewataka kuhakikisha kunakuwa na vipindi vya kuelimisha namna Taasisi inavyotekeleza majukumu yake. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania Profesa Bernadetta Kilian amesema atahakikisha Taasisi inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwamba maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kukidhi matarajio ya watanzania.