Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia na OR - TAMISEMI kwa kushirikiana na Washirika wa
maendeleo leo wamekutana mjini Dodoma kufanya Tathmini ya utekelezaji wa
Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo ( EP4R) kwa mwaka 2016/17 ili kuona
mafanikio yaliyopatikana, changamoto na kuweka mikakati ya kutatua changamoto
zilizopo katika suala la utoaji wa Elimu bora Nchini.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mkutano huo Mratibu wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo
Gerald Mweli kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema
programu hiyo inafanya tathmini ili kujua hali halisi ya utekelezaji wa
majukumu, kwa kiasi gani mradi umefanikiwa lakini pia kuona changamoto na namna
ambavyo serikali kwa kushirikiana na washirika wa watakavyozitatua.
Mweli ametaja
mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo,kuwa ni pamoja na
kujenga na kukarabati miundombinu chakavu ya shule za Msingi na
Sekondari zipatazo 361 kutoka katika Halmashauri 129, vyumba vya mdarasa 1,435,
mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 4, vyoo 2,832, nyumba za walimu 12,
maktaba 4, na uwekaji wa maji katika shule nne (4).
Kwa upande wa vyuo vya
ualimu programu imefanikiwa kukarabati vyuo 10 vya ualimu ikiwa ni pamoja
na kununua compyuta 260 zitakazowawezesha walimu kutekeleza
majukumu yao kwa urahisi, magodoro 6,730 yatakayotumiwa na wanafunzi
pamoja na viti 1976 kwa ajili ya wanachuo.
Aidha, programu
imenunua vifaa vya maabara 1,696 kwa ajili ya shule za sekondari ambavyo
zitasaidia katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na kuongeza uelewa kwa
wanafunzi.