Jamhuri
ya Watu wa Finland imesema itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya Elimu
kwenye eneo la ubunifu ili kuhakikisha vijana wanakuwa wabunifu ili kuweza
kujiajiri pindi wanapomaliza masomo.
Kauli
hiyo imetolewa na Balozi wa Jamhuri ya watu wa Finland nchini Tanzania Pekka
Hukka wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo
jijini Dar es Saalam kuhusiana na namna bora ya utekelezaji wa awamu ya pili ya
programme ya ubunifu inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH).
Waziri
Ndalichako amesema atahakikisha Wizara yake inasimamia kwa karibu utekelezaji
wa programu hiyo ili kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa.
Waziri
Ndalichako amesema Serikali inatambua msaada
ambao umekuwa ukitolewa na Finland katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya Elimu na kuahidi kuwa fedha zitakazotolewa zitatumika kama
zilivyokusudiwa.
Programu
hiyo ya miaka mitano inatarajiwa kuanza
2018 na kukamilika 2022.