Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa kuna baadhi ya wahasibu wa
Wizara hiyo na Taasisi zake ambao wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao kwa
kughushi nyaraka mbalimbali wakati wa kufunga mahesabu kwa lengo la kujipatia fedha
ambazo si halali yao.
Waziri Ndalichako ametoa kauli
hiyo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya uandaaji wa
hesabu za Fedha za Serikali kwa wahasibu wa Wizara hiyo na Taasisi zake.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
akizungumza na Wahasibu wa Wizara hiyo na taasisi zake wakati akifungua mafunzo
ya uandaaji wa hesabu za fedha za serikali jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri
amesisitiza suala la uadilifu, uzalendo na kuwataka wahasibu kuacha kushughushi
nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha ambazo siyo halali yao.
Waziri Ndalichako amesema
Wahasibu wa Wizara lazima wawe mfano katika kuonesha nidhamu kwa kuwa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo Wizara mama kwani kada zote
zinafundishwa na walimu ambao msingi wao ni Wizara hiyo hiyo anayoiongoza.
Waziri Ndalichako ameeleza kuwa kuna
dalili kuwa kuna baadhi ya wahasibu katika Wizara hiyo wanachezea fedha za
Umma, hivyo amewaeleza Wahasibu hao kuwa hivi sasa kuna ukaguzi
unaendelea kwenye Wizara hiyo na matokeo ya ripoti hiyo yatakapokamilika umma
utajulishwa.
“Kuna misemo kuwa eti mbuzi anakula
kwa urefu wa kamba yake, sasa kamba inakatika, tuwe makini na kanuni za kazi,
Fedha za serikali katika awamu hii ya Tano ni sumu, nyaraka nyingi ambazo
zimekuwa zikitumika kwenye kufunga hesabu ni za kughushi, majina yamekuwa
yakijirudia katika semina ambazo zimekuwa zikifanyika, saini tofauti jambo
linaloashiria kuwa kuna wahasibu wanachezea fedha za serikali na huo ni wizi wa
kishamba, amesisitiza Waziri Ndalichako.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Elimu CPA (T) Rose Waniha akizungumza
na wahasibu wakati wa mafunzo ya uandaaji wa fedha za serikali mkoani dar es
salaam
Waziri huyo ameeleza kuwa zipo
pia baadhi ya Taasisi za Wizara hiyo zinapokusanya fedha za ada hawaziingizi
kwenye mfuko wa serikali.
Hivyo ameielekeza Wizara hiyo na
Taasisi zake zote kuhakikisha kuwa hadi itapofika Novemba moja mwaka huu ziwe
zimejiunga na mfumo wa serikali wa malipo ya kielektroniki (GePG- Government e
- payment Gateway Systeam) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya
serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
akizungumza na Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo CPA(T) Rose Waniha wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya uandaaji wa hesabu za Fedha za Serikali, mafunzo hayo ya
siku Tano yameanza leo na yatakamilika oktoba 26, 2018
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa
Wizara hiyo CPA (T) Rose Waniha amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea
uwezo wahasibu kuwa na uelewa wa pamoja wa namna bora ya uandaaji wa
hesabu za fedha za serikali.
Mafunzo hayo ya siku Tano yaliyoanza
leo yatahitimishwa oktoba 26, 2018.
Baadhi ya wahasibu wakifuatilia hotuba ya
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya uandaaji wa hesabu za Fedha za serikali, mafunzo
yanayofanyika jijini Dar es salam.