Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewashauri watumishi wa Bodi ya Mikopo ya
wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za
mikopo ya Wanafunzi kwa njia ya mifumo.
Waziri Ndalichako amesema hayo jijini
Dar Es Salaam alipotembelea ofisi ya HESLB lengo la kujiridhisha na hali ya
mwenendo wa utoaji mikopo kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea
na masomo kwa mwaka 2018/2019.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
(mwenye koti la samawati) akiongea na wateja waliofika Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es Salaam kurejesha madeni yao ya
mikopo ya Elimu ya juu.
Katika ziara hiyo licha ya
kukutana na Menejimenti ya HESLB, Prof. Ndalichako pia aliongea na Katibu
Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) Profesa Charles Kihampa kuhusu hali
ya udahili wa Wanafunzi wa Elimu ya juu ambapo Kihampa alitumia nafasi hiyo pia
kukabidhi orodha ya Wanafunzi 2,600 ambao udahili wao umethibitishwa.
Awali katika
taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa
Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru ilisema kiasi cha shilingi bilioni 98.12 mpaka
sasa kimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 27,929 kati
ya wanafunzi 40,485 wa mwaka wa kwanza waliotarajiwa kupatiwa
mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako (Katikati)
akitambulishwa kwa Maafisa Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul-Razaq Badru.
Badru alisema kuwa idadi ya wanafunzi waliobaki
wapatao 12,556 watapangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni
42 katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyokusudiwa.
Aliongeza
kuwa idadi ya wanafunzi 27,929 waliokwishapangiwa mikopo na
ambao wamedahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vinavyotambulika ni
asilimia 69 ya wanafunzi 40,485 wanaotarajiwa
kunufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019.
Orodha ya
majina ya wanafunzi hao 27,929 (Awamu ya kwanza 25,532 na awamu
ya pili 2,397) waliokwishapangiwa mikopo inapatikana
kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz na itatumwa kwenye vyuo husika kwa
ajili ya hatua zaidi za kukamilisha malipo ya mikopo hiyo.