Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema dhamira ya Serikali ya kumuenzi baba
wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere kwa kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi
na Teknolojia, (MJUNAT) iko palepale.
Waziri Ndalichako ametoa kauli
hiyo akiwa Wilayani Butiama mkoani Mara mara baada ya kutembelea Chuo
hicho kwa lengo la kukagua miundombinu yake, pamoja na kuzungumza na watumishi
wanaofanya kazi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakitoka nje mara
baada ya kukagua bwalo la chakula katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi
na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere.
Akizungumza na Watumishi wa Chuo
hicho pamoja na viongozi wa Mkoa na wale wa Wilaya ya Musoma na Butiama amesema
hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya miundombinu hiyo kutoka
kwa aliyekuwa mmiliki wa majengo hayo Nimrod Mkono.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Moshi
Kabengwe na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia CPA (T) Rose
Waniha wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha Waziri kwenye Chuo Kikuu cha
Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani BUTIAMA
mkoani Mara.
Waziri Ndalichako amesema lengo la
kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ni kumuenzi baba wa Taifa
kwa kutambua mchango wake katika suala la kilimo na kuwa suala hili pia
limeanzishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi.
“Mchakato huu ulianza mwaka 2016
na kuwa hapo awali majengo haya yalikuwa yanamilikiwa na Nimrod Mkono, hivyo
Serikali haiwezi kujenga au kuboresha bila kuwa na maandishi ya kisheria ya
umiliki halali. Napenda kueleza kuwa makabidhiano yako katika hatua za mwisho
ili Serikali iweze kuendelea na taratibu nyingine” alisema Ndalichako.
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
akipokelewa na Watumishi katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia
cha Mwalimu Nyerere, kilichopo Butiama, Mkoani Mara.