Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.William Ole Nasha ameshiriki
shughuli za ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu iliyopo
Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Mhe.Ole
Nasha ameshiriki ujenzi huo na Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani wakati kukagua
miradi ya inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia katika Wilaya
hiyo ambapo amewataka wananchi kuendeleza jitihada hizo ili kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kusoma.
Naibu
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akishiriki
‘Msaragambo’ wa Ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu
iliyoko Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara
kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Wilaya hiyo.
Kufuatia
jitihada hizo za Wananchi Naibu Waziri Ole Nasha amewaahidi wananchi kuwa
Wizara itajenga vyumba viwili vya
madarasa, mabweni mawili na matundu ya vyoo ikiwa ni kuunga mkono juhudi ambazo
wananchi wa kijiji cha Ruvu Darajani wameonesha lakini pia kuwezesha wanafunzi
kutulia shuleni na kusoma.
“Serikali
ikiona eneo ambalo wananchi wameanza na wana hamasa ya kujiletea maendeleo
haiwezi kusita kuja kusaidia, Wilaya ya Same mmeonesha mfano kupitia utaratibu
wenu wa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano hivyo Wizara itaunga mkono juhudi
hizi kwa kuwajengea vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo,” alisema
Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa aelekezo katika
eneo ambalo vyumba viwili vya madarasa vitajengwa katika Shule ya Msingi Ruvu
Iliyoko katika Kata ya Ruvu Darajani Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro.
Naibu
Waziri huyo pia amewataka wananchi wa Kijiji cha Ruvu Darajani ambao
wanajihusisha na shughuli za ufugaji kuacha kutumia watoto kuchunga mifugo
badala yake kuhakikisha wanatumia fursa ya Elimu bure kuwaandikisha watoto wote
waliofikia umri wa kwenda shule.
Awali
Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki alimweleza Naibu Waziri wa Elimu kuwa changamoto
ya upungufu wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Ruvu ambayo imetokana
na ongezeko la Wanafunzi waliohamishiwa shule hiyo kutokana na shule walizokuwa
wakisoma miundombinu yake kuathiriwa na mafuriko yaliyotokana na mvua za masika
za mwaka huu.
Katika ziara hiyo Naibu
Waizri Ole Nasha pia alitembelea shule ya Sekondari Makanya, Chuo cha Maendeleo
ya Wananchi Same na Shule ya Sekondari Same ambapo ameridhishwa na ukarabati
ulivyofanyika katika shule kongwe hiyo .
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua ukarabati wa miundombinu uliofanyika katika Shule ya Sekondari Same iliyoko Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro. Ameridhishwa na namna ukarabati huo ulivyofanyika na kuwataka kutunza miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu.