Jumatatu, 22 Januari 2018

Wizara ya Elimu yatoa msimamo kuhusu Shule kufukuza Wanafunzi kwa kutofikia wastani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi wa wamiliki wa shule binafsi za sekondari ambapo kwa pamoja  wamejadili utekelezaji Wa waraka Namba. 7 unaokataza wanafunzi kufukuzwa shule kwa sababu ya kutofikisha wastani wa ufaulu uliowekwa na shule.

 Waziri Ndalichako ameeleza ameeleza kuwa chimbuko la waraka huo ni baadhi ya shule kufukuza idadi kubwa ya wanafunzi wakiwa Mwaka wa mwisho wa masomo yao kwa kigezo cha kutotimiza wastani unaotakiwa kitendo ambacho amekielezea kuwa kuwa ni cha kibaguzi na ki-unyanyasaji. 

" Mfano  shule ya sekondari Pandahil ambayo imefukuza watoto 148, shule ya sekondari star high imefukuza wanafunzi 49 hizo ni baadhi tu, Aidha, ameeleza kuwa   Wakati Bunge na Serikali ikisikitika pale Wasichana wanapopata uja uzito na kuacha shule, Waja sekondari na Musindi sekondari zimefukuza wanafunzi wa kike 15 kila moja kwa kigezo cha ufaulu mdogo.

Waziri huyo amesisitiza kuwa wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa waraka huo na amewataka Viongozi hao kuweka utaratibu mzuri kwa wanafunzi walio na uwezo mdogo badala ya utaratibu uliopo sasa wa kuwafukuza shule na hivyo kuwaacha wakiwa hawana pa kwenda.

Kwa upande wao viongozi wa wamiliki wa shule wameeleza kuwa utekelezaji wa waraka huo utasababisha kushukuka kwa Ubora Wa ufaulu katika shule zinazomilikiwa na watu binafsi.


Kikao hicho pia kilihudhuriwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo kikao ambacho kimefanyika jijini Dar es salaam.



Jumamosi, 20 Januari 2018

TBA yapewa wiki moja kuanza ujenzi kampasi ya Mloganzila

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameipa wiki moja  Wakala wa Majengo nchin- TBA- Kuhakikisha ujenzi wa majengo mbalimbali  unaanza mara moja ikiwa ni pamoja na kuongeza mafundi pamoja na kupeleka vifaa vya ujenzi katika Mradi wa  Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.

Prof.  Ndalichako ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa, hosteli, ofisi na bwalo la Chakula katika Chuo Kikuu hicho kilichopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambapo amesema hajaridhishwa na kasi ujenzi huo.

Waziri Ndalichako amesema Wizara tayari ilishaipatia TBA kiasi cha shilingi bilioni 3.9 kama malipo ya awali lakini mpaka sasa hakuna jengo lolote ambalo limeshaanza kujengwa na wala hakuna vifaa vya ujenzi katika eneo hilo zaidi ya kuchimbwa misingi tu.

Waziri Ndalichako amesema hatavumilia kuona udahili wa  wanafunzi wa fani za Afya unachelewa katika kampasi hiyo kwa kuwa  lengo la serikali ni kuongeza idadi ya wanafunzi wa fani hizo nchini.


Naye Kaimu Meneja wa Mkoa kutoka TBA Manase Kalage amemwakikisha Waziri kuwa maagizo aliyoyatoa watayatekeleza ikiwa ni pamoja na kukamilisha mradi huo kwa wakati.



Ijumaa, 19 Januari 2018

Waziri Ndalichako aagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu wa Kitengo Cha Manunuzi cha MUHAS

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amemuagiza Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili- MUHAS kumsimamisha kazi Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa Chuo hicho.

Waziri Ndalichako amtoa agizo hilo alipofanya ziara katika Chuo hicho jijini Dar es Salaam ambapo amesema Mkuu wa Kitengo hicho Nuru Mkali amekuwa akikuka taratibu za manunuzi na kupelekea kuwepo Kwa ufisadi mkubwa wa fedha za serikali. 

Aidha, amemtaka Mwenyekiti wa baraza la Chuo hicho Mariam Mwafisi kupitia mikataba yote ya manunuzi kwa miaka mitatu ili kuona watu wote walioshiriki katika mchakato huo mbovu wa manunuzi na endapo itabainika basi hatua za kisheria zichukuliwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la Chuo hicho Mariam Mwafisi amesema wamepokea maelekezo na watayafanyia kazi  ikiwemo kumsimamisha kazi Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi.

Akiwa katika  Chuo cha Taaluma na Tiba kilichopo Mloganzila nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Waziri Ndalichako amemuagiza Makamu Mkuu wa Chuo hicho anaeshughulikia  huduma za Hospitali katika kampasi hiyo Said Abood kuhakikisha anawatembelea  wagonjwa kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabiki pindi wanapokuwa hospitalini hapo.

Prof Ndalichako pamoja na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee  na Watoto  Dkt. Faustine Ndugulile wamefanya ziara katika hositali hiyo ili kujionea changamoto mbalimbali na  namna bora ya kuzipatia ufumbuzi.







Alhamisi, 18 Januari 2018

TBA yaagizwa kukamilisha ukarabati kabla ya Januari 22

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha  inakamilisha ukarabati wa shule za Jangwani na Azania kabla ya Januari  22, mwaka huu ili kuwezesha masomo kuanza.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya  kukagua  Maendeleo ya ukarabti wa  shule hizo.

Waziri ndalichako amesema  ameridhishwa na namna  ukarabati wa shule hizo unavyofanyika, licha ya kuwa bado kuna  kazi kubwa ambayo bado haijafanyika. 

Waziri ameitaka TBA kuhakikisha wanakamilisha miundombinu muhimu mapema ikiwemo madarasa, mabweni, na vyoo ili kuwawezesha wanafunzi kuanza masomo  kabla ya januari 22, mwaka huu.


Kwa upande wake Msanifu Majengo Cecilia Muhongo wa TBA amesema wamejipanga kuhakikisha ukarabati wa miundombinu muhimu itakayowawezesha   wanafunzi kuanza masomo inakamilika mapema.

Jumatatu, 8 Januari 2018

Serikali kuimarisha Elimu Nje ya Mfumo Rasmi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako amesema Mkakati wa Serikali ni kuimarisha Elimu Nje ya Mfumo Rasmi ili kuwapa nafasi watoto wanaoshindwa kujiunga na Mfumo huo wa Elimu kuwa na fursa nyingine ya kupata Elimu na Ujuzi ambao utawasaidia katika kulileea Taifa Maendeleo .

Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam katika ofisi ndogo za Wizara alipokutana na kufanya mazungumzo na  balozi  wa Uingereza Sarah Cooke, balozi wa Sweden katrina Rangnitt na balozi wa Canada Alexandre leveque wanaowakilisha nchi zao hapa nchini
Waziri Ndalichako amewaambia Mabalozi hao kuwa Elimu Nje ya Mfumo usio Rasmi ipo kwa ajili ya kuwasaidia wale walioshindwa  kujiunga na Mfumo Rasmi wa Elimu, hivyo hata wale watakaopata ujauzito wanashauriwa kujiunga katika mfumo huo ili kuendelea na masomo yao mara baada ya kujifungua.

Profesa Ndalichako amesema lengo la serikali ni kuwapa fursa wanafunzi wanaokosa nafasi au wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali waweze kupata Ujuzi na Elimu katika njia nyingine ikiwemo mafunzo ya ufundi katika Vyuo vya Ufundi Stadi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii mafunzo ambayo yatawawezesha kujiajiri ama kuajiriwa.

Akizungumzia Mkakati wa Serikali katika kupambana na changamoto za mtoto wa kike kupata elimu , Profesa Ndalichako alisema mpaka sasa serikali kupitia Programu ya lipa kulingana na Matokeo, EP4R imeshajenga zaidi ya mabweni 300 katika maeneo mbalimbali nchini hasa yale yaliyo katika mazingira magumu na kutoa wito kwa wafadhili mbalimbali kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuchangia ujenzi wa mabweni katika maeneo yenye mazingira magumu kwa  ili kuwasaidia wanafunzi wawezekufanya vizuri katika masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi wengine Balozi wa Sweden nchini Tanzania Katarina Rangnitt amesema wamefurahishwa sana kusikia kutoka kwa Waziri kuwa watoto wanaopata mimba shuleni wanapata fursa nyingine ya kupata Elimu na ujuzi nje ya mfumo usio rasmi ambao utawasaidia katika kuendeleza maisha na kuewa Elimu ndiyo nguzo pekee katika kujieletea Maendeleo.