Jumatano, 16 Mei 2018

EP4R ILIVYOSAIDIA KUONDOA CHANGAMOTO YA MIMBA KWA WANAFUNZI WA KIKE MKOANI LINDI.


Wakuu wa shule za Sekondari mkoani Lindi wamesema kuwa ujenzi wa mabweni unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Lipa Kulingana na matokeo, yaani EP4R katika mkoa huo utasaidia sana kuondoa changamoto ya wananfunzi wa kike kupata mimba wakiwa katika umri mdogo.

Wakizungumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Mkuu wa shule ya sekondari ya Ruangwa Mwalimu Herber Ngonyani amesema kupitia mradi wa EP4R shule hiyo imeweza kujenga mabweni Mawili ambayo yanauwezo wa kuchukua wanafunzi Laki moja na sitini kwa wakati mmoja, huku Mkuu wa shule ya Sekondari Nkowe Ahmed Maliki akikiri kuwa shule yake  imejenga mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi mia moja na ishirini na nane kwa mara moja.
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Ruangwa Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).


Wakuu hao wa shule wameeleza kwa muda mrefu watoto wa kike katika wilaya hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu na hivyo kukumbana na vishawishi ambavyo hupoteza ndoto za wanafunzi hao.

“ Nikiri kuwa mwamako wa Elimu katika Wilaya yetu bado uko chini hivyo hata hamasa ya wazazi na watoto nayo iko chini katika suala zima la Elimu, sasa hiki ambacho Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia inachokitekeleza kupitia mradi wa Lipa kulingana na matokeo kwa kweli ni mkombozi kwa watoto wa kike kwa kuwa sasa watasoma kwa utulivu tena wakiwa katika mazingira ya shule kutokana na ujenzi huu wa mabweni,”anasema Mwalimu Herbert Ngonyani.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Nkowe Ahmed Maliki amessitiza kuwa uwepo wa mabweni utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya utoro miongoni mwa wanafunzi pamoja na kuwasidia wanafunzi wa kike kupuka mazingira hatarishi ya kutembea umbali mrefu takribani kilometa 4 hadi tano kwa siku kwa ajili ya kufika shuleni. 
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Nkowe Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Bweni hilo litasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi wa kike kupata mimba katika umri mdogo.

Mwalimu Malik amesema kuwa mabweni hayo yatasaidia siyo tu kuhuduia wanafunzi wa wanaotoka kwenye mkoa wa Lindi pekee bali wananfunzi kutoka mikoa mbalimbali watanufaika na mabweni hayo.


Katika kutekeleza uboreshaji wa Miundombinu ya shule za msingi, moja ya shule ambazo zilipatiwa fedha za kujenga miundombinu hiyo ni pamoja na shule ya msingi Nangumbu ambayo ilipatiwa kiais cha shilingi Milioni sitini na sita kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na matundu ya vyoo sita lakini shule hiyo imeweza kujenga vyumba vya madarasa vinne, ofisi moja na matundu kumi ya vyoo.

Timu ya wananhabari ambayo imeambatana na maafisa wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kesho itaendelea na ziara yake Mkoani Mtwara ikiwa na lengo la kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari inayotekelezwa kupitia program ya lipa kulingana na matokeo.
Muonekano wa moja ya darasa liliojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Shule ya Sekondari Nkowe iliyopo katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.

Jumatatu, 14 Mei 2018

ZAMBI: AELEZEA EP4R ILIVYOBORESHA MIUNDOMBINU YA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI


  •          AKIRI KUWA SASA SHULE ZIMEKUWA MPYA

Zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetumika kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa wa Lindi na hivyo kuchochea kuongeza kwa kiwango cha ufaulu miongoni mwa wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi wakati akizungumza na timu ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ameeleza kuwa Mpango huo Maalumu wa  Lipa Kulingana na Matokeo yaani EP4R umebadilisha muonekano wa mazingira na kuzifanya shule nyingi za Mkoa huo kuwa mpya.

Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Msingi Kitomanga lililopo katika Halmashauri ya Lindi Vijijini Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 

Zambi amesema kupitia EP4R Mkoa huo umejenga vyumba vya madarasa 30 kwa shule za Msingi, vyumba 22 kwa shule za sekondari, maabara 6 zimekarabatiwa, na ujenzi wa matundu ya vyoo 84 na kuwa ujenzi na michiro ya miundombinu hiyo imekuwa ikizigatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.


Hata hivyo ameeleza kuwa bado ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea katika shule za Msingi na Sekondari ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule mbalimbali.

“Kabla ya ukarabati nikiri kuwa hali ilikuwa siyo nzuri katika miundombinu ya shule lakini kupitia EP4R Mkoa wa Lindi miundombinu yake imebadilika sana ambapo pia imeongeza hamasa ya wanafunzi kusoma na hivyo kuongeza ufaulu, pia utoro umepungua sana maana kuboreka kwa miundombinu kumehamasisha wanafunzi kupenda shule,” anasema Zambi.
1.       Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Sekondari Kilwa lililopo katika Halmashauri ya Lindi Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 

Mkuu huyo wa mMkoa amesema kuwa ukarabati wa maabara kwa Mkoa huo pia umesaidia sana mwitikio wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kuwa hivi sasa wanafanya mazoezi kwa vitendo na hivyo kuwafanya waelewe kwa urahisi.

Mkuu huyo wa mkoa amekiri kuwa bado mwitikio wa Elimu katika Mkoa  huo uko chini na hivyo kuwafanya watoto walio wengi kutothamini Elimu.

“Mwitikio wa wananchi kuhusu Elimu bado uko chini, na wazazi ndiyo wanaochangia kwa kuwa ndiyo wanaowapeleka watoto wao kwenda kufanya shughuli za shambani ikiwemo kutuma korosho pamoja na kushiriki katika masuala ya mila na tamaduni za kuwapeleka watoto kwenye unyago,” anasema Zambi.
 Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Msingi Masoko lililopo katika  Halmashauri ya Kilwa Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 


Mkuu huyo amesisitiza kuwa ni vyema wazazi wakatambua umuhimu wa Elimu ili kuwasaidia watoto kupenda shule kwa lengo la kuliletea taifa Maendeleo.

Timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali pamoja na Maafisa kutoka Kitengo Cha Mawasiliano Cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wako Mkoani Lindi kwa ajili ya kufuatilia uboreshaji wa miundombinu inayojengwa na kukarabatiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo, EP4R.

Mikoa mingine ambayo timu hiyo itafanya ufuatiliaji ni pamoja na Mkoa wa Mtwara na Songea.
1.       Muonekano wa jingo la Choo kilichojengwa katika Shule ya Msingi Kitomanga iliyopo Wilayani Lindi Vijijini Mkoani Lindi, Ujenzi choo hicho umetekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).

PROF. NDALICHAKO: TUMIENI FURSA YA FEDHA ZA UMOJA WA ULAYA KATIKA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Taasisi za Kitafiti, Vyuo Vikuu na watu mbalimbali ambao wanahusika na  kufanya tafiti katika masuala ya uchumi pamoja na usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kufanya tatiti zenye tija.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na  wageni waliofika kushuhudia uzinduzi rasmi wa wito kwa ajili ya maandiko ya kuomba fedha kiasi cha uro milioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania bilioni nne zilizotolewa na Umoja wa Ulaya.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa wito kwa ajili ya maandiko ya kuomba fedha kiasi cha uro milioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania bilioni nne zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kwa lengo la kuwezesha tafiti hizo ili kuiwezesha serikali kusimamia raslimali za nchi katika kuleta tija na kuisaidia serikali ya awamu ya tano  kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini na Afrika Mashariki Roeland Van de Geer amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kusaidia watafiti, Vyuo Vikuu na Mashirika ya Kitafiti yasiyokuwa ya kiserikali kwa kuwa ni wachangiaji wa mijadala ya kisera kupitia matokeo ya tafiti wanazofanya  katika kuleta mabadiliko ya uchumi wa viwanda na kuondoa umasikini.

Ijumaa, 11 Mei 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA: LESENI ZA BIASHARA SI KIGEZO CHA MWANAFUNZI KUPATA MKOPO ELIMU YA JUU.Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema kumiliki biashara au kuwa na leseni ya biashara si kigezo cha kuamua kama mwanafunzi anastahili kupata mkopo au asipate mkopo

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mijini Dodoma kufuatia taarifa ambazo zimesambaa kwenye vyombo mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii zikieleza kuwa wafanyabiashara wenye leseni watoto wao hawatapata mikopo kwa ajili ya Elimu ya Juu.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani mjini Dodoma kutolea ufafanuzi kuhusu vigezo vinavyotumika katika  kutoa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. 

Amesisitizama kinachoangaliwa ni kipato ambacho mzazi au mlezi anakipata katika kazi anayoifanya kama kinaweza kumgharamia mtoto wake masomo ya Elimu ya Juu na sio kazi anayoifanya.
Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wananchi kupuuza taarifa hizo za uongo na upotoshaji zenye lengo la kuvuruga utaratibu uliopo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha wakati akitolea ufafanuzi kuhusu vigezo vinavyotumika kutoa Mkopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu leo Mjini Dodoma.

Jumatano, 9 Mei 2018

DK. SEMAKAFU AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA UNICEF


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu leo amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka UNICEF kwa lengo la kujengeana uelewa wa pamoja juu ya kile wanachokitekeleza kuhusuiana na Sekta ya Elimu.

Mazungunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara Jijini Dodoma ambapo wote kwa pamoja wamekubaliana kuimarisha mawasiliano ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu katika sekta hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akisisitiza jambo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Timu ya Ujumbe kutoka UNICEF juu ya namna bora ya kutekeleza majukumu ya kielimu katika Sekta hiyo.

Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF wanatekeleza shughuli za kielimu katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songea, Kigoma na Tabora kwa kutoa mafunzo kwa waratibu Elimu Kata, mafunzo kwa walimu kazini kuhusu Elimu Jumuishi, lishe, uongozi na utawala kwenye Elimu. 


Kikao hicho pia kimejumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu na Timu ya Ujumbe kutoka UNICEF, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakiwa katika mazungumzo ya namna bora ya kutekeleza shughuli za kielimu za Sekta hiyo.

WAZIRI NDALICHAKO: MAABARA YA KISASA INAYOJENGWA TANZANIA KUDHIIBTI MIONZI NCHI ZA AFRIKA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako Leo ametembelea na kukagua hatua za mwisho za usimikaji wa vifaa mbalimbali ndani ya maabara ya kisasa ya Kuhakiki vifaa vinavyopima mionzi katika Tume ya nguvu za Atomiki- TAEC iliyopo mkoani Arusha.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maabara hiyo Waziri Ndalichako amesema serikali imejenga maabara hiyo ya kisasa ili kudhibiti masuala ya mionzi kwa nchi za Afrika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea maelezo kuhusu usimikaji wa vifaa vya kisasa katika maabara ya nyuklia kwenye Tume ya nguvu za Atomiki iliyoko mkoani Arusha.

Alisema maabara hiyo ambayo sasa ipo katika hatua za kufungwa vifaa mbalimbali vya kisasa itawezesha nchi mbalimbali kuja kujifunza namna ya kupima masuala mbalimbali ya mionzi.

Waziri Ndalichako amesema kuwa hadi sasa serikali imeshatoa kiasi cha sh. bilioni 2.38 huku Umoja wa Ulaya (EU) ikitoa vifaa vyenye thamani ya sh.  bilioni 11.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia kwa karibu moja ya kifaa kilichosimikwa kwa ajili ya upimaji wa mionzi kwenye maabara ya kisasa ya nyuklia kwenye Tume ya nguvu za Atomiki, TAEC mkoani Arusha.

Ijumaa, 4 Mei 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:  info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz
  
Chuo cha Masomo ya  Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA          

Tarehe:  4 Mei, 2018

TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa na taarifa za upotoshaji ambazo zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii, ambazo zinaonesha dosari na makosa katika vitabu. Mojawapo ni picha inayoelezea viungo vya mwili wa mwanadamu na nyingine iko katika Kitabu cha Kiingereza chenye maneno yanayosomeka “The Big City of Tanzania”.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutarifu umma kuwa kitabu kinachosambazwa kinachoelezea viungo vya mwili wa mwanadamu si chapisho la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na wala si miongoni mwa vitabu ambavyo vimesambazwa kwenye shule. Kitabu hicho hakina uhusiano wowote na wala hakifanani na vitabu ambavyo vimechapishwa hivi karibuni na TET.
Aidha, kuhusu kitabu cha Kiingereza, hilo ni chapisho la mwaka 2016 ambalo limefanyiwa marekebisho katika chapisho la mwaka 2018.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inawasihi watanzania kupuuza taarifa hizo ambazo siyo za kweli na zina nia ya kupotosha na kuleta usumbufu kwa jamii. Wizara pia inatumia fursa hii kuwakumbusha wananchi kuzingatia Sheria za Matumizi ya Mitandao na kutambua kuwa kutoa taarifa za uongo ni kosa la jinai.
                                                  Imetolewa na:      
Mwasu Sware
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
04/05/2018