Jumapili, 2 Juni 2019

CHUO KIKUU MZUMBE CHATIKIWA KUWEKA UTARATIBU MZURI ILI KUWEZESHA WANAFUNZI KUPATA MIKOPO KWA WAKATI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameanza ziara za kukutana na wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kupokea na kusikiliza maoni, mapendekezo na changamoto za wanafunzi hao kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi.
Waziri Ndalichako ameanza ziara hiyo katika Chuo Kikuu Mzumbe akiwa ameambatana na viongozi kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ambapo ameuagiza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kuandaa utaratibu utakaohakikisha wanafunzi wanaojitokeza kusaini nyaraka za mikopo mapema kuwezeshwa kupata fedha zao kwa wakati.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungmza na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
“Hili jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanasaini kwa wakati nakupa Rais wa wanafunzi, uwahamasishe wenzako kusaini mapema ili wapatiwe fedha kwa kuwa serikali haina tatizo la fedha na ndio sababu zinapelekwa kwa wakati katika Vyuo,” alisisitiza Waziri Prof. Ndalichako.
Awali, baadhi ya wanafunzi walimweleza Waziri kuwa wanachelewa kupokea fedha za mikopo zinazopelekwa chuoni hapo na serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kupata taarifa.
Ili kutatua changamoto zilizopo katika kupatikana kwa mikopo kwa wakati wanafunzi hao walipendekeza kuwepo kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya Serikali ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo na kuzitafutia uvumbuzi kwa pamoja.
Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Hayupo Pichani) wakati wa ziara yake ya kutembelea vyuo Vikuu na kuzungumza na wanafunzi
Akitoa ufafanuzi, Makamu Mkuu wa chuo Prof. Lugano Kusiluka amesema Menejimenti ya chuo hicho imekua ikikutana na changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutojitokeza kusaini nyaraka zinazohitajika kuthibitisha uwepo wao chuoni licha ya kukumbushwa mara kwa mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Prof. Charles Kihampa wameahidi kutoa ushirikiano kwa menejimenti za vyuo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mikopo kwa wakati.

Ijumaa, 31 Mei 2019

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA UJUZI


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Tate-Ole Nasha amefunga rasmi maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ambapo ameilielekeza baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kuhakikisha maonesho hayo yanafanyika angalau kwa mwaka mara moja.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema kuwa Elimu ya Ufundi ni nyenzo inayomsaidia mtu kupambana na changamoto ikiwemo kujiajiri na siyo kusubiria kuajiriwa, hivyo kupitia mafunzo ya ufundi yanawaandaa wahitimu kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha.

Mhe. Ole Nasha amesema Serikali ya awamu ya Tano inapozungumzia Tanzania ya viwanda ni pamoja na kujiandaa kuhakikisha inakuwa na wataalamu wenye stadi na ujuzi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungmza na wananchi (Hawapo Pichani)  wa Dodoma wakati wa kufunga maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyofanyika Jijini Dodoma
“Katika kufikia uchumi wa viwanda Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika kujiletea Maendeleo, na ili kufikia lengo hilo ni lazima tuwe na wataalamu wa kutosha ambao watasaidia kutatua changamoto mbalimbali,”alisistiza Mhe. Ole Nasha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Prof. John Kondoro amesema madhumuni ya maonesho hayo ni kutangaza Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu miongoni mwa washiriki.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu AveMaria Semakafu wakisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Skauti anayeshiriki katika Maonesho ya Kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yaliyoratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo.
Prof. Kondoro amesema miongoni mwa changamoto ni pamoja na muda wa maandalizi kuwa mfupi na hivyo washiriki wengi kushindwa kujipanga na kuja kushiriki ameahidi kuwa baraza litajipanga ili kutoa fursa kwa washiriki wengi zaidi kushiriki katika maonyesho yajayo.

Kauli mbiu ni “Elimu ya Ufundi na Mafunzo kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na mmoja wa washiriki wa maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo wakati alipotembelea maonesho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma

WAZIRI NDALICHAKO AKIPONGEZA CHUO KIKUU MZUMBE KWA USIMAMIZI MZURI WA UJENZI WA HOSTELI ZA WANAFUNZI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako  amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa hosteli za wanafunzi unaoendelea Chuoni hapo.
Waziri Ndalichako ametoa pongezi hizo Mkoani Morogoro wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi unaoendelea Chuoni hapo ambapo amesema ameridhishwa na kasi na ubora wa majengo yanayojengwa

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiongozana na Viongozi pamoja na wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa hosteli za wanafunzi unaoendelea katika Chuo Kikuu Mzumbe wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
Mradi huo unaogharimu Shilingi bilioni 6.5 unahusisha ujenzi wa Majengo manne ya ghorofa ya hosteli za wanafunzi ambayo yatachukua wanafunzi 1,024 kwa mara moja pindi yatakapokamilika. Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa nyumba za waangalizi pamoja na maeneo ya kufulia na kuanikia nguo za wanafunzi.
Aidha,Waziri Ndalichako ametoa pongezi kwa SUMA JKT kwa kutekeleza mradi huo kwa kasi na kwa ubora huku akiwataka wakandarasi wengine wanaofanya kazi katika miradi mbalimbali ya ujenzi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuiga mfano wa SUMA JKT katika utendaji.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikaga baadhi ya majengo ya hosteli za wanafunzi yanayoendelea kujengwa katika Chuo Kikuu Mzumbe. Mradi huo unafadhiliwa na serikali. 
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kuboresha miundo mbinu ya Chuo hicho katika Kampasi ya Mbeya na Kampasi Kuu Morogoro, akieleza kuwa uwekezaji wa kiasi hicho kwa Chuo Kikuu Mzumbe haujafanyika kwa zaidi ya miaka 40.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikapata maelezo juu yamradi wa ujenzi wa hoasteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu Mzumbe .

Jumanne, 28 Mei 2019

MAONESHO YA KWANZA YA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YAZINDULIWA DODOMA


Serikali imesema imetenga kiasi cha shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kujenga Chuo cha Ufundi kipya katika makao makuu ya nchini, jijini Dodoma.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo, mjini Dodoma.

Waziri Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuimarisha vyuo vya kati, kuhuisha mitaala ili kuendana na Teknolojia, ambapo tayari serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi Stadi nchini.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akihutumia washiriki wa maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo pamoja na wananchi wa jiji la Dodoma (Hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Maonesho hayo.

Waziri amevitaka vyuo vyote vya ufundi nchini kuzingatia taratibu, kanuni na sheria katika kuendesha vyuo hivyo na yeyeote ambaye hatakidhi vigezo basi chuo hicho kitanyang’anywa ithibati.

“Zoezi la ukaguzi kwa vyuo vya Ufundi ni endelevu, hivyo vyuo ni lazima vizingatie taratibu, kanuni na  sheria , na chuo ambacho  hatakidhi vigezo kitanyang’anywa ithibati.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la Uongozi wa baraza la Taifa la Ufundi (NACTE), Prof. John Kondoro amesema vyuo vilivyoshiriki ni zaidi ya 100 ambapo washiriki watapata fursa ya kukuza ushirikiano miongoni mwao.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo ya  baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na wanafunzi kutoka moja ya chuo kinachoshiriki katika maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo Jijini la Dodoma.

Prof.Kondoro amesema ndani ya miaka miwili serikali imesaidia kuweza kukaguliwa kwa vyuo vyote 500 vya ufundi vilivyopo nchini Jambo ambalo halikwahi kufanyika katika miaka ya nyuma.

Prof. Kandoro amesema maonesho hayo ni jukwa la kukutanisha wadau, kutangaza na kuona namna watu wanavyoweza kujiajiri na siyo kusubiria kuajiriwa.
Waziri wa Elimu, Sayannsi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kuhusu gari linalotumia gesi lililobuniwa na wataalamu kutoka Chuo cha Ufundi Dar es Salaam (DIT) lililopo katika maonesho ya kwanza ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo yanayofanyika  jiji la Dodoma.

Ijumaa, 24 Mei 2019

BALOZI FINLAND AIPONGEZA WIZARA YA ELIMU KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI


Balozi wa Finland Pekka Makka ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Elimu inayofadhiliwa na Finland ambayo imewezesha uboreshaji katika maeneo mbalimbali  ya sekta hiyo.

Balozi Makka ametoa pongezi hizo jijini Dodoma alipofika ofisi za Wizara na kukutana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake ambapo amesema kupitia utekelezaji wa miradi hiyo wameiona sekta ya elimu ikiboreshwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akisalimiana na Balozi wa Finland Pekka Makka  alipofika ofisi za Wizara kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake.
Makka amesema Wizara ya elimu imeboresha miundombinu katika shule mbalimbali nchini na kuweka mazingira mazuri ya wanafunzi kujifunza, huku akipongeza walimu kwa kuboresha mbinu za ufundishaji.  

Balozi huyo amesema Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uboreshaji wa sekta ya elimu hususan katika maeneo ya Elimu ya Ufundi, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kupanua wigo wa upatikanaji wa mafunzo nchini.

“Tumeona maboresho makubwa katika sekta ya elimu, nasi kama wafadhili tumefarijika na hakika tunaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendelea kuboresha sekta hii muhimu, na ninaahidi kuwa Balozi anayekuja kunipokea ataendeleza ushirikiano huu,” amesema Makka.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na Balozi wa Finland Pekka Makka  alipofika ofisi za Wizara kwa lengo la kushukuru kwa ushirikiano pamoja na kuaga baada ya kumaliza muda wake ambapo ameipongeza wizara kwa kutekeleza vyema miradi mbalimbali.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameishukuru Finland kwa ufadhili  wa Euro milioni 52 kwa ajili ya miradi, ambapo amesema kupitia ufadhili huo Tanzania imeshirikiana na Finland kuongeza fursa za elimu na mafunzo kwa  elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu  Wazima, hususan kwa kuwajengea uwezo watekelezaji wa mpango wa ‘Intergrated Post Primary Education (IPPE)’ na mpango wa ‘Intergrated Programme for Out of School Adolescents (IPOSA)’.  

Miradi mingine aliyoitaja ambayo imefadhiliwa na Finland ni pamoja  elimu ya afya na michezo katika vyuo vya ualimu ambayo ililenga kuwajengea maarifa na ujuzi wakufunzi  na walimu tarajali waweze kufundisha shuleni kwa kuzingatia umuhimu wa michezo shuleni na kwa maendeleo ya taifa, mradi wa Tehama, (TANZAICT) unaotekelezwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), mradi ambao umewezesha kuwepo na mifumo ya kukuza ubunifu na kuwezesha mfuko wa kufadhili wabunifu wadogo.

Aidha, Naibu Waziri amesema ushirikiano kati ya Wizara na Finland utakaoendelea unalenga zaidi katika Mafunzo ya Ufundi na Ubunifu na kwamba umekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia viwanda.

“Ili kufikia uchumi wa kati  kupitia viwanda ni lazima tuwe na rasilimaliwatu ya kutosha iliyoelimika na yenye maarifa na ujuzi kwa ajili ya viwanda na pia itakayoweza kujiajiri,” amesisitiza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Balozi wa Finland Pekka Makka  wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa wizara mara baada ya kikao na Balozi huyo.



Jumatano, 22 Mei 2019

WIZARA YA ELIMU YAKUTANA NA UJUMBE TOKA CHINA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Avemaria Semakafu ameongoza majadiliano kati ya Wizara na Ujumbe kutoka taasisi ya China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center ya nchini China yaliyolenga kutambua maeneo ya kushirikiana na nchi hiyo katika Sekta ya Elimu na jinsi ambavyo elimu kupitia teknolojia inaweza kuchangia moja kwa moja kwenye uchumi wa viwanda.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Uongozi wa Wizara na viongozi kutoka taasisi mbalimbali za nchini China ambazo zinajihusisha na masuala mbalimbali ikiwemo Tehama.  Ujumbe huo kutoka China uliongozwa na Mkurugenzi wa taasisi ya China-Africa Industrial Cooperation Promotion Center, Bw. Wenbao Tan.

Katika majadiliano hayo wamekubaliana kuona uwezekano wa kushirikiana katika maeneo ya ufundishaji wa lugha ya Kichina katika vyuo vya ualimu na ufundi, uanzishwaji wa maabara za kufundishia lugha, uboreshaji mifumo ya elimu mtandao pamoja na uanzishwaji wa hospitali ya kujifunzia.
Ujio huo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maeneo makuu ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya China na Afrika yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Afrika Kusini mwaka 2015.