Jumatano, 15 Agosti 2018

SERIKALI KUJENGA MAJENGO MAPYA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA

Serikali imesema itajenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga ili kukihamisha kutoka  kwenye majengo ya Kanisa Katoliki ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa mkoani  Rukwa kwenye ziara  ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo amesema kwa sasa ni vigumu kufanyia ukarabati majengo yanayotumika kwa sababu si maliya serikali.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wanachuo, Wakufunzi na Wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga (Hawapo pichani) ambapo serikali imeahidi kujenga majengo mapya kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga

Waziri Ndalichako amesema suala la uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho lipo ingawa changamoto iliyopo ya eneo pamoja na majengo kuwa si mali ya chuo hicho na kwamba kanisa Katoliki wanalihitaji eneo hilo kwa matumizi mengine.

“Chuo Cha Ualimu Sumbawanga hakijasahaulika katika kufanyiwa ukarabati, changamoto iliyopo ni kuwa eneo hili mlikaribishwa lakini mkang’ang’ania sasa wenyewe wanataka eneo lao ” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Aidha Waziri amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha shilingi bilioni 36 kimetengwa kwa  ajili ya kuvifanyia ukarabati vyuo saba vya Ualimu, huku Chuo Cha   Ualimu Murutunguru na Kabanga vikitarajia kujengwa upya.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea taarifa ya Mkoa wa Rukwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalifan Haule mara baada ya kufanya ziara ya Kikazi katika mkoa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amesema anawashukuru Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga kwa kuruhusu Chuo hicho kufanya shughuli zake katika eneo lake kwa muda mrefu, kwani mwanzoni kanisa hilo lilijenga majengo hayo ili kwa lengo la kuanzisha chuo cha kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema tayari  mkoa wake umeshatafuta eneo lingine ambalo Chuo hicho kitahamishiwa, na kuwa hivi sasa tayari Mkoa  umesharatibu taratibu  za kuanza kulipa fidia kwa wakazi ambao eneo Lao litachukuliwa kwa ajili ya matumizi ya Chuo hicho.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo akimuonyesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako baadhi ya majengo ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga









Alhamisi, 9 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AIAGIZA NACTE KUFUNGIA VYUO VINAVYOTOA MAFUNZO KWA UBABAISHAJI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuendelea kufungia vyuo vinavyotoa  mafunzo kwa ubabaishaji  ili kulinda ubora wa Elimu na Ujuzi kwa wanafunzi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizindua Baraza la Uongozi la Taifa la Elimu ya Ufundi ambapo amewataka NACTE kufungia hata vyuo  vya serikali kama itabainika kutoa mafunzo yasiyo na ubora.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Baraza la Baraza la Uongozi la Taifa la Elimu ya Ufundi Prof. John Kondoro Sheria na Kanuni za Baraza hilo wakati wa uzindzi uliofanyika jijini Dar es Salaam

“Hatutaki kuwa na utitiri wa vyuo vingi ni bora kuwa na vichache lakini vitoe wahitimu wenye ujuzi na maarifa ambao wanaweza kuwa na mchango katika Taifa letu.” Amesisitiza Waziri Nalichako.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo akizungumza na wananchi wa mtaa wa Majimatitu B Kata ya Kilungule mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya shule mpya inayojengwa kwa ajili ya kupunguza mlundikano wa wanafunzi wa shule ya msingi Majimatitu A 

Pia Waziri Ndalichako amekagua Maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya Msingi inayojengwa Majimatitu Wilayani Temeke  yenye lengo la  kupunguza mlundikano wa wanafunzi katika shule ya Msingi Majimatitu A yenye wanafunzi zaidi ya 7000.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua madaftari ya wanafunzi wa Darasa la pili katika shule ya Msingi ya Majimatitu A. Waziri Ndalichako alifika shuleni hapo kujionea mrundikano wa wanafunzi katika shule hiyo

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI MAAFISA WATATU WA WIZARA YA ELIMU.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Joyce  Ndalichako  amemuagiza  Katibu  Mkuu wa Wizara hiyo  Dk. Leonard Akwilapo kumsimamisha kazi Afisa manunuzi  Audifasy Myonga na watumishi wengine wawil wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo mkoani Morogoro baada ya kutembelea chuo Cha Ualimu Morogoro  na kukuta idadi kubwa ya vifaa vya maabara visivyotumika huku muda wa matumizi ya vifaa hivyo  ukikaribia kuisha muda wake wa matumizi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro ambapo amekuta vifaa na madawa ya maabara ambayo yamehifadhiwa bila kutumika tangu mwaka 2016.
Ndalichako amesema ununuzi wa vifaa hivyo unaonyesha kuwa na shaka kwani vifaa hivyo vilinunuliwa kwa awamu mbili ndani ya mwezi mmoja huku gharama ya manunuzi ikionyesha kupanda mara mbili hadi tatu kutoka gharama ya awali.

“Mkuu wa Chuo ameeleza vizuri kabisa kuwa vifaa hivyo vilinunuliwa bila wao kushirikishwa, sasa unajiuliza mnunuzi amewezeje kununua vifaa vya maabara bila kuwashirikisha watumiaji,” alihoji Waziri Ndalichako .
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro. Waziri pia alisikiliza changamoy=to walizonazo watumishi hao. 

Pia, Waziri Ndalichako  ametembelea shule ya Sekondari ya Mzumbe kwa lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa na wizara ambapo amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao ili wafaulu kwa viwango vya juu.



Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu wakikagua baadhi ya miundombinu iliyokarabatiwa katika shule ya Sekondari Mzumbe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Jumatano, 8 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA BODI YA HUDUMA ZA MAKTABA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Bodi mpya ya Huduma za Maktaba Tanzania kuhakikisha inaanzisha Maktaba za Wilaya ili kuwawezesha watanzania wengi kunufaika na Elimu na Maarifa yatokanayo na usomaji wa vitabu.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi hiyo na kusisitiza kuwa kuwepo kwa maktaba hizo kutaondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata maktaba za mikoa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Prof. Rwekaza Mkandala Sheria za Bodi hiyo. 

“Wananchi wanapenda kusoma vitabu sasa natoa rai kwenu Bodi mpya mshirikiane na Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa kuanzisha Maktaba katika Wilaya zote, sisi kama Serikali tutaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha tunaimarisha utoaji wa huduma za maktaba nchini.” Alisisitiza Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti wa Baraza laUsimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Naomi Katunzi Sheria za Bodi hiyo. Ameiagiza Baraza hilo kuweka vigezo vitakavyotumika kutoa Elimu nje ya mfumo rasmi.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ametemblea Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na kuzindua Baraza la Usimamizi la Taasisi hiyo ambapo amelitaka  baraza hilo kuboresha vigezo vinavyotumika kusajili vituo vinavyotoa Elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi pamoja na kusimamia ubora wa elimu inayotolewa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiongea na Watumishi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (Hawapo Pichani) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Jumatatu, 6 Agosti 2018

AWAMU YA PILI MAFUNZO UTHIBITI UBORA YAANZA KATIKA KANDA TANO


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza awamu ya pili ya kutoa mafunzo kwa Wathibiti Ubora  wa shule kwa Kanda za Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Morogoro  na Mtwara juu ya  kutekeleza mfumo mpya wa Uthibiti ubora wa shule.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wathibiti ubora mkoani Arusha Naibu Waziri William Ole Nasha amewataka watumishi hao kusimamia mfumo na mxhakato wa utoaji wa Elimu kwa kuhakikisha Sera, kanuni , sheria na mongozo inazingatiwa na wadau wote katika sekta ya Elimu.

Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya wathibiti ubora awamu ya pili yanayoendelea nchini.

 Naibu waziri ole Nasha amewataka wathibiti ubora kuhakikisha dhamira ya serikali inatimizwa kwa wathibiti ubora wa shule kuhama kutoka katika dhana ya ukaguzi kama wajuaji zaidi, au polisi kwa kukagua zaidi na badala yake wawe wathibiti ubora wa shule  kwa kuhakikisha kuwa wanawasaidia walimu, kwa lengo la kuhakikisha serikali inafikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.


Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa wizara hiyo, Euphrasia Buchuma amefungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam ambapo amewataka Wathibiti Ubora kuzingati mafunzo yanayotolewa ili kuwawezesha kufanyia kazi  yale yote yanayoelekezwa.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi ya Mfumo Mpya wa Uthibiti Ubora wa Shule wakimsikiliza Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchumu (Hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa shule ya sekobdari Zanaki Jijini Dar es Salaam

Buchuma amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wathibiti ubora wa shule kuweza kufanya  ukaguzi wa shule kwa kutumia mfumo mpya ambao ni shirikishi unaoangalia zaidi tendo la kujifunza, kufundisha na kufanya upimaji katika ngazi ya darasa.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo  mthibiti ubora wa shule  kutoka Manispaa ya Ilala Diana Justine amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutatua changamoto wanazokuta nazo  shuleni kwa kushirikiana na walimu, wanafunzi na jamii tofauti na awali walipokuwa wanakwenda kuangalia matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo hayo.

Jumapili, 5 Agosti 2018

NDALICHAKO ATAKA SHULE YA SEKONDARI MANGA DELTA KUPANDISHA TAALUMA


Waziri wa Elimu, Sayamsi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amewataka walimu wa shule ya sekondari Manga Delta iliyoko wilayani Kibiti mkoani Pwani kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi kimasomo ili taaluma katika shule hiyo iweze  kupanda.

Waziri Ndalichako ametoa agiza hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule hiyo ambapo amesema hajaridhishwa na mwenendo wa taaluma katika shule hiyo.

Amesema pamoja na serikali kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo bado imekuwa ikishuka kitaaluma mwaka hadi mwaka.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalich ako akizungumza na wanafunzi, walimu na wazaza wa shule ya Sekondari Manga Delta iliyoko wilayani Kibiti mkoani Pwani. Waziri Ndalichako amewataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi kimasomo ili taaluma katika shule hiyo iweze  kupanda.

 “Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi milioni 256 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa na bweni juhudi hizi ziende sambamba na ufundishaji ili taaluma ipande”  Alisisitiza Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi ufunguo wa pikipiki kwa mmoja wa Waratibu Elimu Kata ambapo amekabidhi Pikipiki kumi na sita katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Kibiti Mkoani Pani. Waziri Ndalichako amewataka Waratibu Elimu Kata hao kutumia Pikipiki hizo katika shughuli zitakazosaidia kuboresha Elimu.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kila mwezi imekuwa ikitoa kiasi cha silingi bilioni 20. 8 kugharamia Elimu bila malipo pamoja na kutoa shilingi laki mbili na nusu za posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata hivyo amewataka kuwajibika ili kupandisha taaluma ya shule hiyo.

Waziri wa Elimu amehitimisha ziara yake ya siku mbili ya kikazi wilayani Kibiti mkoni Pwani kwa kukabidhi gari ya Idara ya Udhibiti Ubora kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo pamoja na pikipiki kumi na sita kwa Waratibu Elimu Kata.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifungua gari kabla ya kumkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kibiti Alvera Ndabagoye kwa ajili ya Idara ya Udhibiti Ubora ya wilaya hiyo. Waziri Ndalichako amewataka Wadhibiti ubora nchini kufanya kazi zao kwa weledi

SHULE YA MSINGI KIOMBONI KUJENGEWA MIUNDOMBINU MIPYA


Waziri wa Elimu, Sayamsi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amehaidi kujenga na kuboresha miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Kiomboni ambayo miundombinu yake kwa sasa ni chakavu.  

Waziri Ndalichako ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule hiyo iliyopo katika Kijiji cha Kiomboni Kata Salawe Wilayani Kibiti Mkoani Pwani.

Amesema kuwa shule hiyo pamoja na kuwa chakavu ina upungufu wa vyumba vya madarasa hvyo kupelekea hali ya ufundishaji na ujifunzaji kuwa ngumu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikaribishwa na baadhi ya viongozi na wananchi wa Kijiji wa Kiomboni Wilayani Kibiti mkoani Pwani alipowasili katika kijiji hicho ili kujionea changamoto zinazoikabili shule ya msingi ya Kiomboni. Waziri Ndalichako aliwahaidi wanakijiji hao kuwa serikali kupitia wizara yake watajenga miundombinu mipya katika shule hiyo

"Nimezinguka katika shule hii nimejionea kwa macho yangu jinsi miundombinu yake ilivyo kwenye hali mbaya na ninaahidi kuwa wizara yangu itafanya uboreshaji wa miundombinu hii ili mazingira ya kujifunzia yaweze kuwavutia watoto kupenda shule  " Aesema Ndalichako.

Waziri huyo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamilia kuboresha miundombinu ya Shule kwa kukarabati na kujenga mipya ili kuwezesha watoto kjifunza katika mazingira rafiki.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na viongozi wa wilaya ya Kibiti wakikagua miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo  ya shule ya msingi kiomboni ambayo yamechakaa. Waziri huyo yupo wilayani Kibiti katika ziala ya kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa na wizara ya elimu kupitia programu ya EP4R

Ndalichako amewahakikishia walimu wa shule hiyo pamoja na wanakijiji kuwa ujenzi na Ukarabati huo utafanyika mapema kabla ya mvua za masika hazijaanza.

Awali katika taarifa yake Mkuu wa shule Musa Mapange  alimweleza Waziri kuwa Shule hiyo haina vyoo imara kwani vilivyokuwepo vimeharibika na kufungwa na sasa watoto wanajisaidia katika vyoo vilivyotengenezwa kwa dharula.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Mbunge wa Kibiti Ali Ungando na Mkuu wa Wilaya hiyo Philiberto Sanga wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule  msingi kiomboni. Ndalichako  amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

Waziri Ndalichako upo katika ziara ya siku mbili ya kikazi Wilayani Kibiti mkoani Pwaniku kagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na wizara Kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)